Iran yaonya kuziandama benki za Marekani, Israel
11 Machi 2026
Mapema asubuhi ya Jumatano (Machi 11), droni mbili zinazodaiwa kurushwa na Iran ziliangukia karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dubai, ambapo watu wanne walijeruhiwa.
Hata hivyo, shughuli za safari kwenye uwanja huo ziliendelea kuwa za kawaida, kwa mujibu wa Ofisi ya Habari ya Dubai.
Kabla ya hapo, kombora jengine liliipiga meli iliyobeba makontena kwenye Mlango Bahari wa Hormuz, ambapo moto mkubwa ulizuka na kuwalazimisha mabaharia wake kujiokowa, kwa mujibu wa jeshi la Uingereza.
Nchini Kuwait, serikali ilisema mifumo yake ya ulinzi wa anga ilikuwa imefanikiwa kuzidunguwa droni nane za Iran.
Nayo Saudi Arabia iilsema iliweza kuzidunguwa droni tano zilizokuwa zinaelekea kwenye visima vyake vya mafuta vya Shaybah.
Mlango wa Hormuz wafungwa
Iran inatajwa kufanikiwa kusimamisha safari za meli za mizigo kwenye Mlango Bahari wa Hormuz, ambako robo moja ya mafuta yote ya dunia kutokea Ghuba ya Uajemi hupitia kuelekea Bahari ya Hindi.
Pia imekuwa ikivilenga visima na mitambo ya kusafishia mafuta kwenye mataifa jirani ya Ghuba, kwa lengo la kuweka mbinyo wa kilimwengu dhidi ya uchokozi ulioanzishwa na Marekani na Israel mwishoni mwa mwezi wa Februari.
Kamandi yake ya pamoja ya kijeshi ya Iran ilisema siku ya Jumatano kuwa benki na taasisi za masuala ya fedha zingelianza kuwa sehemu ya maeneo yatakayoandamwa na mashambulizi yake.
Makao Makuu ya Khatam al-Anbiya ilitowa taarifa hiyo baada ya vyombo vya habari vya Iran kuripoti kwamba mfanyakazi mmoja wa beki mjini Tehran aliuawa kutokana na mashambulizi ya Marekani na Israel.
"Kutokana na mashambulizi haya haramu na yasiyokubalika, adui anatulazimisha kuvilenga vituo vya kiuchumi na benki zenye mafungamano na tawala za Kizayuni na Marekani kwenye eneo hili," Ebrahim Zolfaqari, msemaji wa kamandi hiyo alisema akiwaonya raia kukaa mbali na benki na taasisi zote za kifedha.
Israel yashambulia Tehran, Lebanon
Kwa upande wake, Israel ilisema ilikuwa inaendelea na mashambulizi yake dhidi ya Tehran kufuatia mashambulizi ya Jumanne ambayo wakaazi wa huko waliyaelezea kuwa makubwa kabisa tangu uchokozi uanze.
Miripuko ilisikika siku ya Jumatano mjini Beirut na kusini mwa Lebanon, ambako Israel ilidai kulilenga kundi la Hizbullah lenye mafungamano na Iran.
Jengo moja katika kiunga cha Aisha Bakar mjini Beirut liliporomoka baada ya mashambulizi hayo, ingawa hadi sasa hakuna taarifa za watu waliouawa.
Kabla ya hapo, mashambulizi kwenye wilaya ya Nabatieh kusini mwa Lebanon yaliwauwa watu watano na wengine wawili waliuawa kwenye wilaya za Tyre na Bint Jbeil.
Tangu Hizbullah ilipojiunga rasmi na vita vilivyoanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran mwanzoni mwa mwezi huu, mashambulizi ya Israel yameshauwa karibuni watu 500 nchini Lebanon, wengi wao wakiwa raia wa kawaida.