Iran yapatiwa pendekezo jipya juu ya mpango wake wa nuklea
3 Mei 2008Taarifa hiyo imetolewa na waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Miliband kwa waandishi wa habari kufuatia mazungumzo mjini London na mawaziri wenzake wa Ujerumani, Urusi China,Ufaransa na Marekani.
Miliband amesema mpango huo wa marupurupu ni sehemu ya mkakati wenye pande mbili katika kushughulikia suala la mpango tata wa nuklea wa Iran.Amesema maelezo kamili juu y mpango huo hayatotangazwa hadharani.
Kwa upande wake waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema leo hii wanachotaka mataifa hayo ni kwa Iran kusitisha tu urutubishaji wa uranium katika kipindi hiki cha mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mzozo wa nuklea na nchi hiyo.
Mataifa mengi ya magharibi yanahofu kwamba Iran inaweza kuwa inataka kutengeneza silaha za nuklea hata hivyo Iran yenyewe imekuwa ikisisitiza kwamba mpango huo ni kwa ajili ya dhamira ya amani tu.