1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano mapya yaifungulia Iran soko la mafuta duniani

Iddi Ssessanga ape,afpe,rtre
17 Juni 2026

Rasimu iliyovuja ya makubaliano kati ya Marekani na Iran inaonyesha kuwa Tehran itaruhusiwa kuuza mafuta bila vikwazo, kupata dola bilioni 300 za ujenzi baada ya vita kwa kubadilishana na kufunguliwa Mlango wa Hormuz.

Ujerumani 2026 | Mahusiano ya Iran na Marekani: Kwa nini hawawezi kuwa marafiki?
Mahusiano ya Iran na Marekani: Kwa nini hawawezi kuwa marafiki?Picha: DW

Rasimu ya makubaliano kati ya Marekani na Iran yanayotarajiwa kusainiwa nchini Uswisi Ijumaa imeibua mjadala mkubwa duniani baada ya taarifa kuonyesha kuwa Tehran itaruhusiwa kuuza mafuta yake bila vikwazo mara moja na kufungua tena Mlango Bahari wa Hormuz.

Nakala za makubaliano zilizochapishwa na kituo cha televisheni cha Al Arabiya na kuthibitishwa kwa kiasi kikubwa na maafisa kadhaa wa Mashariki ya Kati zinaonyesha kuwa pande hizo mbili zimekubaliana kusitisha uhasama na kuanza mazungumzo ya siku 60 kuhusu makubaliano ya kudumu ya mpango wa nyuklia wa Iran.

Iwapo makubaliano hayo yatatiwa saini kama yalivyo sasa, yatakuwa miongoni mwa makubaliano makubwa zaidi kuwahi kufikiwa kati ya Washington na Tehran tangu mapinduzi ya Iran ya mwaka 1979.

Makubaliano hayo yanakuja miezi kadhaa baada ya vita vilivyozuka kati ya Marekani, Israel na Iran, ambavyo vilisababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu, vifo vya mamia ya watu na mtikisiko katika soko la nishati duniani.

Kwa mujibu wa rasimu hiyo, pande zote zimekubaliana kusitisha mara moja na kwa kudumu mapigano yote, ikiwa ni pamoja na yale yanayoihusisha Lebanon na kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran.

Mwanamke akiwa akiwa ameshika bendera ya Iran karibu na bango linaloipinga Marekani lenye picha ya Rais Donald Trump na Mlango Bahari wa HormuzPicha: Majid Asgaripour/WANA/REUTERS

Hormuz kufunguliwa tena na biashara kurejea

Moja ya vipengele muhimu zaidi vya makubaliano hayo ni kufunguliwa tena kwa Mlango Bahari wa Hormuz, njia nyembamba inayounganisha Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman.

Kabla ya vita, takribani asilimia 20 ya mafuta yote yanayouzwa duniani yalipitia katika njia hiyo. Kufungwa kwake kulisababisha kupanda kwa bei za mafuta, gesi na bidhaa nyingi katika masoko ya kimataifa.

Kwa mujibu wa rasimu hiyo, Iran itachukua hatua za haraka kurejesha usafirishaji wa kawaida wa meli za kibiashara katika kipindi cha siku 30 na kusaidia kuondoa mabomu ya majini yaliyowekwa wakati wa vita.

Marekani nayo imekubali kuondoa vizuizi vya kijeshi vilivyowekwa katika bandari za Iran na kusaidia kurejesha shughuli za usafirishaji katika kiwango kilichokuwepo kabla ya vita.

Wachambuzi wa uchumi wanaona hatua hiyo kama habari njema kwa uchumi wa dunia uliotikiswa na mgogoro wa nishati uliofuatia kufungwa kwa Hormuz.

Iran inavyoweza kujilinda dhidi ya mashambulizi ya Marekani

01:42

This browser does not support the video element.

Iran yapewa nafasi ya kuuza mafuta

Makubaliano hayo pia yanaonyesha kuwa Wizara ya Fedha ya Marekani itatoa vibali maalumu vinavyoruhusu Iran kuuza mafuta ghafi, bidhaa za petrokemikali na bidhaa nyingine zinazotokana na mafuta mara baada ya makubaliano kusainiwa.

Hatua hiyo ni muhimu kwa sababu mauzo ya mafuta ndiyo chanzo kikubwa zaidi cha mapato ya serikali ya Iran. Kwa miaka mingi Tehran imekuwa ikikabiliwa na vikwazo vilivyopunguza uwezo wake wa kuuza mafuta katika soko la dunia.

Wakosoaji wa makubaliano hayo wanasema Marekani imeikabidhi Iran moja ya faida kubwa zaidi kabla hata ya kufikiwa kwa makubaliano ya mwisho kuhusu mpango wake wa nyuklia.

Tofauti na makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015, ambapo vikwazo viliondolewa baada ya hatua kadhaa za Iran kutekelezwa, safari hii baadhi ya manufaa yanaonekana kutolewa mapema zaidi.

Mbali na mafuta, rasimu hiyo inaeleza kuwa Marekani itaanza mchakato wa kuruhusu fedha na mali za Iran zilizozuiwa katika benki mbalimbali duniani kupatikana tena.

Matarajio yanaongezeka nchini Iran kwamba makubaliano mapya na Marekani yatachangia kuimarika kwa uchumi kupitia biashara, mauzo ya nishati na kuachiliwa kwa mali na fedha zilizokuwa zimezuiwa nje ya nchiPicha: picture alliance/Zoonar

Dola bilioni 300 za ujenzi na ahadi za nyuklia

Kipengele kingine kilichozua mjadala ni mpango wa kuhakikisha angalau dola bilioni 300 zinapatikana kwa ajili ya ujenzi na kufufua uchumi wa Iran baada ya vita.

Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance amesema sehemu kubwa ya fedha hizo zinatarajiwa kutoka kwa uwekezaji wa nchi za Kiarabu za Ghuba badala ya walipa kodi wa Marekani.

Makubaliano hayo pia yanaeleza kuwa Iran inasisitiza msimamo wake wa kutotengeneza silaha za nyuklia. Hata hivyo, suala la hatima ya urani iliyorutubishwa na kiwango cha shughuli za nyuklia za Iran litaamuliwa katika mazungumzo yajayo.

Pande hizo mbili zimepewa siku 60 za kujadili makubaliano ya mwisho, huku muda huo ukiruhusiwa kuongezwa kwa ridhaa ya pande zote.

Katika kipindi hicho, Iran itaendelea na hali ilivyo sasa katika shughuli zake za nyuklia, huku Marekani ikiahidi kutoweka vikwazo vipya wala kuongeza uwepo wake wa kijeshi katika eneo hilo.

Iran: Mashambulizi, Kauli tata na Hatma Isiyoeleweka!

18:39

This browser does not support the video element.

Changamoto kwa Netanyahu na maswali yanayosalia

Makubaliano hayo yanatazamwa kama ushindi mkubwa wa kidiplomasia kwa Rais Donald Trump, ambaye amekuwa akitafuta njia ya kumaliza vita na kuzuia mgogoro mkubwa zaidi katika Mashariki ya Kati.

Hata hivyo, kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, rasimu hiyo inaweza kuwa pigo kubwa la kisiasa. Netanyahu alikuwa amehalalisha vita kwa madai ya kuzuia Iran kuendeleza mpango wake wa nyuklia na kudhoofisha washirika wake wa kikanda.

Wachambuzi wengi wanaona kuwa makubaliano hayo hayajafikia baadhi ya malengo makubwa yaliyotangazwa mwanzoni mwa vita, ikiwemo kusitishwa kabisa kwa shughuli za urutubishaji urani au kusambaratishwa kwa makundi yanayoungwa mkono na Iran katika eneo hilo.

Zaidi ya hayo, White House bado haijachapisha rasmi maandishi ya makubaliano hayo na Iran nayo haijatoa nakala yake kamili. Hivyo baadhi ya vipengele vinaweza kubadilika kabla ya kutiwa saini rasmi nchini Uswisi.

Hata hivyo, ikiwa rasimu iliyovuja itaakisi makubaliano ya mwisho, dunia inaweza kuwa inashuhudia mwanzo wa sura mpya katika mahusiano kati ya Marekani na Iran, pamoja na mabadiliko makubwa katika siasa na uchumi wa Mashariki ya Kati.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW