1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yapuuza miito ya kutoishambulia Israel

13 Agosti 2024

Iran imeukataa wito wa mataifa ya Magharibi wa kuacha vitisho vyake vya kulipiza kisasi dhidi ya Israel kwa mauaji ya kiongozi wa kisiasa wa kundi la Hamas, Ismail Haniyeh.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Nasser Kanaani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Nasser KanaaniPicha: Iranian Foreign Ministry/Zuma/picture alliance

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Nasser Kanaani, amesema Jumanne kuwa wito wa Ufaransa, Ujerumani na Uingereza hauna mantiki, wala mashiko ya kisiasa na unakinzana na kanuni za sheria za kimataifa. 

Kwa mujibu wa Kanaani, wito wa mataifa hayo ambao haukulaani uhalifu wa kimataifa unaofanywa na Israel, unaitaka Iran isichukue hatua zozote za kuizuia Israel ambayo imekiuka uhuru wa mamlaka ya eneo lake.

Iran yadhamiria kuzuia mashambulizi ya Israel

Amesema Iran imedhamiria kuzuia mashambulizi ya Israel na kutoa wito kwa Ufaransa, Ujerumani na Uingereza kupinga vita vya Gaza na Israel ambayo inachochea vita.

"Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutochukua hatua na uungaji mkono mkubwa wa kisiasa na kijeshi wa serikali za Magharibi kwa utawala wa Israel, ndiyo sababu kuu zinazoufanya mzozo wa Gaza kutanuka na kuwa wa kikanda," alisisitiza Kanaani.

Majengo yakiwa yameharibiwa kwa mashambulizi ya Israel huko Khan YunisPicha: Rizek Abdeljawad/Xinhua/IMAGO

Katika taarifa yake ya jana Jumatatu, Marekani na washirika wake wa Ulaya ziliitolea wito Iran na washirika wake kujizuia na mashambulizi dhidi ya Israel, na kuepusha kutanuka kwa mzozo.

Iran na washirika wake makundi ya Hamas na Hezbollah la Lebanon, wameishutumu Israel kwa kufanya mauaji ya Haniyeh. Hata hivyo, serikali ya Israel haijakiri kuhusika na mauaji hayo.

Mauaji ya mwanaume wa Kipalestina

Wakati huo huo, wanajeshi wa Israel wamemuua kwa kumpiga risasi mwanaume wa Kipalestina wakati wa msako mkali wa kuvunja makaazi ya washukiwa wawili wa Kipalestina waliokuwa wamezuiliwa mapema Jumanne alfajiri katika Ukingo wa Magharibi, kwenye miji ya Ramallah na Al-Bireh.

Jeshi la Israel halikuweza kuthibitisha mara moja taarifa hizo zilizotolewa na maafisa wa wizara ya afya ya Palestina, pamoja na shirika la habari la Kipalestina la Wafa, ingawa imesema inazifuatilia kwa undani.

Tingatinga la Israel likibomoa makaazi ya Wapalestina katika Ukingo wa MagharibiPicha: Mussa Issa Qawasma/REUTERS

Shirika linalofuatilia wafungwa wa Kipalestina, limesema kuwa mwanaume huyo aliyeuawa mwenye umri wa miaka 18, aliachiliwa huru Novemba 25, wakati wa makubaliano ya kusitisha mapigano kwa wiki moja, yaliyoshuhudia Wapalestina wengi wakiachiliwa huru kutoka kwenye magereza ya Israel na kubadilisha na mateka wa Israel waliokuwa wakishikiliwa huko Gaza tangu Oktoba 7.

Soma zaidi: Mauaji ya Wapalestina Ukingo wa Magharibi

Katika hatua nyingine, wizara ya afya ya Palestina imesema vikosi vya Israel jana Jumatatu vilimuuwa mwanaume mwingine wa Kipalestina karibu na mji wa Azzun mashariki mwa mji wa Qalqilya. Kwa mujibu wa wizara hiyo, aliyeuawa alitambuliwa kama Tariq Ziad Abdul Rahim Daoud.

Jeshi la Israel limesema kuwa awali mwanaume huyo alimfyatulia risasi raia wa Israel huko Qalqilya. Baadae Hamas ilitoa taarifa yake ikiomboleza kifo cha Tariq Daoud, ikisema alikuwa mmoja wa wapiganaji wake.

(AFP, DPA, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW