1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaridhia IAEA kuendelea kukagua vituo vya nyuklia

12 Septemba 2021

Iran leo Jumapili imeridhia kuwaruhusu waangalizi wa kimataifa kuweka vifaa vya kutunza kumbukumbu kwenye kamera kadhaa za kufuatilia nyendo kwenye vituo vyake muhimu vya nishati ya nyuklia.

Rafael Grossi in Iran, Einigung
Picha: FARARU

Tangazo hilo limetolewa na mkuu wa shirika la atomiki nchini Iran Mohammad Eslami baada ya kufanya mkutano na mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kudhibiti matumizi ya nishati ya nyuklia, IAEA, Rafael Grossi aliye ziarani mjini Tehran.

Uamuzi huo huenda utaepusha msuguano wa kidiplomasia ulioshuhudiwa tangu tarehe za mwanzo za mwezi Septemba.

Hata hivyo uamuzi huo bado hautakuwa na mabadiliko makubwa ya uangalizi na unaiacha IAEA kwenye hali ile ile iliyojitokeza mwezi Februari.

Hali hiyo ni kwamba Iran itaendelea kuhodhi mikanda yote ya video inayorikodiwa kwenye vituo vyake vya nyuklia wakati mazungumzo ya kuzishawishi Jamhuri hiyo ya Kiislamu na Marekani kurejea kwenye mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 zikiwa zimeambulia patupu.

Grossi: Uamuzi wenye kuleta faraja

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Nguvu za Atomiki, IAEA, Rafael Grossi akiwa mjini TerhanPicha: WANA/Reuters

Hivi sasa Iran inarutubisha kiwango kidogo cha madini ya Urani lakini kinachokaribia ubora wa juu kabisa unaowezesha kutumika kuunda silaha na akiba yake ya madini hayo yaliyorutubisha inaendelea kuongezeka.

``Ninafarijika kusema kwamba leo tumefanikiwa kupata matokeo muhimu, ambayo yanahusu kuendelea kwa kazi za vifaa vya shirika letu hapa" amesema Grossi. "Ni wajibu wetu kuhakikisha tunaendelea kutoa uhakika na taarifa kwa IAEA na kwa ulimwengu kwamba kila kitu kinakwenda sawa."

Eslami ameyaelezea mashauriano kati ya Iran na shirika la IAEA lenye makao yake mjini Vienna ya "kitaalamu" yasiyohitaji siasa. Pia amesema Grossi atarejea nchini Iran kwa mazungumzo na maafisa wa nchi hiyo bila hata hivyo kutoa ufafanuzi zaidi.

Kadhalika haijafahamika iwapo Iran itakabidhi mikanda ya video iliyorikodiwa miezi iliyopita ambayo serikali mjini Tehran ilikwishatishia kuiharibu.

"Kadi za kutunza kumbukumbu zinafungwa vizuri na kuhifadhiwa nchini Iran kama ilivyo kawaida," amesema Eslami na kuongeza kuwa "Kadi mpya za kutunza kumbukumbu zitawekwa kwenye kamera."

Taarifa ya pamoja kati ya IAEA na Iran imethibitisha maelezo hayo, ikisema suala na njia na wakati wa kukusanya taarifa kutoka vituo vya nyuklia ndiyo linajadiliwa na kukubaliwa na pande zote mbili.

IAEA: Ukaguzi nchini Iran umetatizika tangu Februari

Picha: Alex Halada/AFP/Getty Images

Tangazo hilo la Jumapili bila shaka litaipa Iran muda wa ziada kuelekea kikao cha Bodi ya shirika la IAEA kitakachofanyika wiki inayokuja ambacho tayari mataifa ya magharibi yametia shinikizo la kuikabili Iran kwa kutoonesha ushirikiano kwa wakaguzi wa kimataifa.

Eslami amesema Iran itashiriki kikao hicho na mazungumzo yake na IAEA yataendea wakati wa mkutano huo.

IAEA tayari imeyafahamisha mataifa wanachama wa shirika hilo kupitia ripoti yake ya kila robo ya mwaka iliyotolewa wiki iliyopita kwamba shughuli zake za ukaguzi na ufuatiliaji nchini Iran zimeingia ganzi tangu mwezi Februari baada ya Tehran kuwazuia wakaguzi wake kuifikia mifumo na vifaa vya ufuatiliaji wa shughuli kwenye vituo vya nyuklia.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW