Iran yasema itakutana na Marekani jijini Geneva Alhamisi
23 Februari 2026
Akizungumza na televisheni ya Marekani ya CBS News, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amesema maelezo ya uwezekano wa makubaliano yanaandaliwa kabla ya mazungumzo mapya kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran. "Ikiwa wanataka kupata suluhu kwa ajili ya mpango wa nyuklia wa amani wa Iran, njia pekee ni diplomasia. Na tumethibitisha hili huko nyuma, na naamini kwamba bado, kuna nafasi nzuri ya kuwa na suluhisho la kidiplomasia ambalo litakuwa na faida kwa pande zote mbili, na tunaweza kufikia suluhisho. Kwa hivyo hakuna haja ya vitisho vyovyote vya kijeshi. Kukusanya zana za kijeshi hakuwezi kusaidia, na hakuwezi kutushinikiza."
Araghchi amesema "Ikiwa Marekani itawashambulia, basi wana kila haki ya kujilinda." Hata hivyo, alisema, "kuna nafasi nzuri ya kuwa na suluhisho la kidiplomasia".
Naye waziri wa mambo ya nje wa Oman ambayo ni mpatanishi mkuu, Badr Albusaidi, amesema mazungumzo yataanza tena Alhamisi mjini Geneva "kwa msukumo chanya wa kuchukua hatua za ziada kuelekea kukamilisha makubaliano hayo". Katika ujumbe wa mitandao ya kijamii, Rais Masoud Pezeshkian wa Iran pia alisema mazungumzo ya awali "yalitoa ishara za kutia moyo".
Haya yote ni baada ya mjumbe wa Washington katika Mashariki ya Kati Steve Witkoff kuiambia televisheni ya Marekani ya Fox News kuwa rais Donald Trump anajiuliza ni kwa nini Iran bado "haijasalimu amri" kutokana na shinikizo. "Kwa nini chini ya shinikizo la aina hii, pamoja na kiasi cha nguvu za kijeshi za baharini, manowari tulizonazo huko, kwa nini hawajatujia na kusema, 'Tunakiri kwamba hatutaki kuwa -- hatutaki kutengeneza bomu. Kwa hivyo hiki ndicho tulicho tayari kufanya.' Na bado ni vigumu kuwafikisha mahali hapo."
Vitisho vya Marekani vya kuchukua hatua za kijeshi vimeongezeka tangu maandamano ya kitaifa nchini Iran yaliposababisha ukandamizaji mkali ambao makundi ya haki za binadamu yanasema uliwaua maelfu ya watu.
Siku ya Jumapili, wanafunzi wa Iran walifanya maandamano yanayokinzana ya kuunga mkono na kupinga serikali, huku wakosoaji wa uongozi wakikabiliwa na hatari ya kukamatwa.
Baada ya duru ya majadiliano ya hivi karibuni huko Geneva, Iran ilisema inaandaa rasimu ya pendekezo la makubaliano ambayo yataepusha hatua za kijeshi.
Serikali za Magharibi zinahofia mpango wa nyuklia wa Iran unalenga kutengeneza bomu, jambo ambalo Tehran imekuwa ikilikana kwa muda mrefu, ingawa inasisitiza haki yake ya kurutubisha urani kwa madhumuni ya kiraia kwa maana ya kutengeneza nishati.
Chanzo: Mashirika