Iran yasema inapitia mapendekezo ya Marekani
21 Mei 2026
Msemaji wa wizara za mambo ya kigeni ya Iran Esmaeil Baqaei amesema jamhuri hiyo ya kiislamu inayafanyia kazi mapendekezo ya Washington waliyoyapokea kupitia nchi mpatanishi ambayo ni Pakistan.
Afisa huyo amerejea matwaka ya Iran ikiwa ni pamoja na kuachiwa kwa mali za nchi hiyo zinazoshikiliwa ughaibuni na Marekani kusitisha mzingiro unaozuia shughuli za bandari nchini Iran.
Mapema jana Jumatano, mkuu wa ujumbe wa Iran kwenye mazungumzo ya kumaliza vita, Mohammad Bagher Ghalibaf aliituhumu Marekani kutaka kuanzisha tena vita baada ya Rais Donald Trump kusema ataishambulia tena dola hiyo ya uajemi iwapo itakataa kufikia mkataba wa amani.
Trump aliwaambia waandishi habari kwamba anaamini wamo kwenye hatua za mwisho za majadiliano na Iran na akaonya ikiwa makubaliano hayatofikiwa mambo yatakuwa magumu kwa watawala mjini Tehran.
"Jambo hilo limekaribia ukingoni. Niamini, kama hatutopata majibu sahihi, mambo yatakwenda haraka sana. Tuko tayari. Ni lazima tupate majibu sahihi. Lazima yawe majibu sahihi kwa asilimia 100. Na tukifanya hivyo, tutaokoa muda, nguvu na maisha.", amesema Trump.
Trump alikwishasema mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa ataishambulia Iran iwapo makubaliano hayatafikiwa. Mwanzoni mwa wiki hii pia alidai kuwa amesitisha mpango wa kuishambulia Iran siku ya Jumanne baada ya viongozi kadhaa wa nchi za Mashariki ya Kati kumrai aishambulie Iran.
Iran yashupalia msimamo, Trump na Netanyahu ´Hamkani si Shwari´
Viongozi wa Iran wamebakia kuwa na misimamo isiyoyumba wakisisitiza kuwa tayari kwa vita lakini kwa upande mwingine wanasema milango ya diplomasia iko wazi.
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema "njia za kufikia suluhisho la kidiplomasia ziko wazi" lakini akatoa hadhari akisema "kuilazimisha Iran kusalimu amri kupitia mabavu ni jambo lisilowezekana na ni njozi ya mchana"
Katika hatua nyingine Jarida la Wall Street limeripoti juu ya mabishano yaliyotokea kati ya Rais Trump na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu walipozungumza kwa njia ya simu siku ya Jumanne kuhusu namna ya kusonga mbele na suala la Iran.
Vyanzo vinasema tofauti kubwa imekuwa ni mtazamo usioshabihiana juu ya pendekezo jipya ya Marekani la kumaliza vita. Pendekezo hilo ambalo inaarifiwa limetokana na ushauri wa mataifa mawili Qatar na Pakistan lina lengo la kupunguza tofauti kati ya Washington na Tehran.
Hata hivyo Netanyahu ameendelea kuwa na mtazamo hasi kuhusu mazungumzo akitaka waanzishe tena mashambulizi ya pamoja na Marekani ili kuidhoofisha zaidi Iran jambo ambalo inatajwa Trump haliungi mkono moja kwa moja.