Iran yasema itajenga upya vituo vya nyuklia
2 Novemba 2025
Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amesema hivi leo Jumapili kwamba nchi yake itajenga upya vituo vyake vya nyuklia, taarifa ya kiongozi huyo inakuja miezi kadhaa baada ya Marekani kuvishambulia vituo vyake vya Nyuklia kwa madai kwamba vilikuwa sehemu ya mpango unaolenga kutengeneza silaha za nyuklia.
Pezeshkian akiwa katika ziara yake kwenye shirika la nishati ya atomiki nchini mwake amesema watajenga vituo hivyo tena kwa nguvu zaidi ingawa hawalengi kuunda silaha za nyuklia.
Rais wa Marekani Donald Trump alionya kwamba nchi yake itafanya mashambulizi mapya dhidi ya maeneo ya nyuklia ya Iran iwapo nchi hiyo ya Ghuba itajaribu kujenga upya vituo ambavyo Marekani ilivishambulia mwezi Juni.
Tehran imeendelea kusisisitiza kwamba mpango wake wa nyuklia ni kwa madhumuni ya kiraia pekee.