Iran: Marekani na Israel bado zina nia ya kupindua nchi
27 Mei 2026
Wizara ya Ujasusi ya Iran imesema leo kwamba Marekani pamoja na Israel bado zina lengo la kuipindua Jamhuri ya Kiislamu na kuigawa nchi hiyo.
Katika taarifa iliyotolewa na kunukuliwa na vyombo vya habari vya Iran, wizara hiyo ilisema kuwa maadui sasa wanajaribu kufanikisha malengo yao kupitia mbinu nyingine baada ya kushindwa kuyatimiza kwa njia ya mashambulizi ya kijeshi. Ilieleza kuwa mpango huo wa kuipindua serikali na kuigawa nchi, ulitangazwa wazi mwanzoni mwa vita hivyo, lakini haukufanikiwa.
Wizara hiyo imeongeza kuwa imepokea taarifa za kijasusi zikidai kuwa Marekani na Israel zinapanga kuongeza shinikizo la kiuchumi, kuchochea migawanyiko ya kidini na kikabila ndani ya Iran, pamoja na kutekeleza hujuma na kile ilichokiita operesheni za kigaidi.
Matamshi hayo yanajiri wakati Iran na Marekani zikiendelea kubadilishana kauli katika juhudi za kusaka makubaliano ya kumalizavita vilivyozuka Februari 28 na kuenea katika eneo la Mashariki ya Kati.