Iran yasema mashambulizi ya Israel ni tangazo la vita
13 Juni 2025
Rais Pezeshkian amesema taifa na viongozi wa Iran hawatanyamaza kimya kutokana na kitendo hicho cha jinai.
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Araghchi, amesema mashambulizi ya anga ya Israel nchini humo yanachukuliwa na Iran kuwa tangazo la vita.
Taharuki duniani kuhusu mashambulizi ya Israel
Shirika la habari la serikali IRNA, limemnukuu Araghchi akisema kuwa Israel imevuka mipaka. Pia ametoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kushughulikia hali hiyo haraka iwezekanavyo.
Wakati huo huo, kiongozi wa mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, ameitishia Israel kwamba itapata adhabu kali.
Khamenei amethibitisha vifo vya makamanda na wanasayansi kadhaa na kuwaita mashahidi.
Amesema mashambulizi hayo ya Israel ambayo pia yalilenga makazi ya watu, yamefichua uovu wa Israel kuliko awali.