1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaiwekea Iran vikwazo vipya

Yusra Buwayhid
25 Juni 2019

Iran Jumanne imelaani hatua za rais wa Marekani Donald Trump za kuiwekea nchi hiyo vikwazo vipya ambavyo vitamlenga zaidi kiongozi wa kidini nchini humo pamoja na viongozi wengine.

USA Washington Donald Trump unterschreibt Executive Order zu Iran
Picha: picture-alliance/AP Photo/A. Brandon

Trump alisaini vikwazo hivyo vipya dhidi ya Ayatollah Ali Khamenei na washirika wake Jumatatu. Maafisa wa Marekani wamesema wamepanga pia kumuwekea vikwazo Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Javad Zarif. 

"Baada ya muda mfupi, nitasaini amri ya kutekeleza vikwazo vigumu dhidi ya Kiongozi wa Kidini wa Iran pamoja na viongozi wengine wengi. Hatua ya leo inafuatia mfululizo wa vitendo vya kikatili vya serikali ya Iran katika wiki za hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na kuangusha ndege ya Marekani isiyotumia rubani. Nadhani kila mtu kaliona hilo na mengine mengi," alisema Trump akizungumza na waandishi habari kabla ya kusaini amri hiyo.

Shirika la habari la serikali nchini Iran IRNA Jumanne limemnukuu msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran Abbas Musavi akisema kwamba hatua alizochukua Trump zinamaanisha mwisho wa diplomasia kati ya nchi hizo mbili.

Iran itaendelea kutozingatia majukumu yake

Musavi aliongeza kwamba serikali ya Iran itaendelea kutozingatia majukumu yake chini ya makubaliano ya nyuklia yaliyoafikiwa mwaka 2015 kati ya Iran na nchi tano wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Uingereza, Ufaransa, Urusi, China pamoja na Marekani ambayo baadae ilijiondoa chini ya utawala wa Trump.

Kiongozi wa Kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei Picha: picture-alliance/AP Photo/Office of the Iranian Supreme Leader

Marekani imesema imechukua hatua hizo kuizuia Iran na mpango wake wa kutengeneza silaha za nyuklea pamoja na kuunga mkono makundi ya wanamgambo.

Matamshi ya Mousavi ni sawa na ya balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa Majid Takht Ravanchi, aliyeonya jana kwamba hali katika Ghuba ya Uajemi ni ya hatari sana na kwamba hakuwezekani kufanyika mazungumzo, huku Marekani ikiendelea kuiwekea Iran vikwazo pamoja na vitisho.

Trump mwaka jana aliiwekea tena vikwazo Iran baada ya kuiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015, yaliyoafikiwa chini ya uongozi wa rais wa zamani Barack Obama. Na duru hii ya pili ya vikwazo itazuia fedha za Khamenea na viongozi wengine wa kijeshi wa Iran ambazo ziko chini ya mamlaka ya Marekani.

Trump amesema vikwazo hivyo vipya sio tu kwasababu ya kuangushwa kwa ndege isiyo na rubani ya Marekani. Marekani pia inailaumu Iran kwa mashambulizi ya meli mbili za kubebea mafuta yaliyotokea mwezi huu katika Mlango wa bahari wa Hormuz.

Soma zaidi: Iran yakanusha madai ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani

Chanzo: (ap,dpa)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW