1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Iran: Wanachama 28 wa kundi la kigaidi la "IS" wakamatwa

24 Septemba 2023

Mamlaka nchini Iran imesema leo kuwa imewakamata watu 28 wanaohusishwa na kundi linalojiita dola la kiislamu IS kwa kupanga njama ya kuilenga Tehran wakati wa kumbukumbu ya maandamano baada ya kifo cha Mahsa Amini.

Iran Soldaten
Picha: Iranian Army/AA/picture alliance

Mahsa Amini ni mwanamke wa umri wa miaka 22 aliyekufa chini ya kizuizi cha polisi wa maadili mnamo Septemba 16, 2022, baada ya kukamatwa kwa madai ya kukiuka sheria kali za mavazi ya wanawake nchini humo.

Taarifa iliyochapishwa katika tovuti ya wizara inayohusika na masuala ya ujasusi, imesema katika siku za hivi karibuni, wakati wa operesheni katika maeneo ya Tehran, huko Alborz na Azabajani Magharibi, nyumba na maeneo kadhaa ya magaidi yalishambuliwa na wanachama 28 wa mtandao huo wa kigaidi walikamatwa.

Taarifa hiyo imeendelea kusema kwamba watu hao wa wanahusishwa na kundi la kigaidi la Daesh na baadhi yao wana historia ya kuandamana na wapiganaji wa jihadi nchini Syria ama kufanya shughuli zao nchini Afghanistan, Pakistan na eneo la Kurdistan nchini Iraq.

Wizara hiyo imesema kuwa maafisa wawili wa usalama walijeruhiwa wakati wa operesheni hiyo na mabonu kadhaa, silaha, fulana za kujitoa mhanga na vifaa vya mawasiliano vilikamatwa.