Iran yashambulia tena Bahrain na Kuwait
6 Juni 2026
Iran imevurumisha makombora dhidi ya washirika wa Marekani, Bahrain na Kuwait baada ya mashambulizi mapya ya Marekani, hatua iliyoubua hasira kubwa katika falme za Ghuba na kutishia kusambaratisha usitishaji mapigano dhaifu uliopo.
Jeshi la Marekani limesema makombora saba yalirushwa, sita yakidunguliwa huku moja likianguka kabla ya kufika shabaha. Bahrain na Kuwait zimeyataja mashambulizi hayo, ambayo ni ya pili ndani ya siku tatu, kuwa uchokozi wa wazi na tishio kwa usalama wa raia.
Iran imesema ililenga "kambi za adui” kujibu operesheni za Marekani dhidi ya maeneo yake, lakini Marekani imesema hakuna wanajeshi wake waliojeruhiwa na imekanusha madai ya uharibifu wa makao ya Kikosi cha Tano cha Jeshi la Wanamaji nchini Bahrain.
Mashambulizi yamesikika karibu na uwanja wa ndege wa Kuwait na katika mji mkuu wa Bahrain, huku wakazi wakieleza hofu baada ya milipuko mikubwa. Juhudi za kidiplomasia za kuimarisha usitishaji vita zinaendelea kukwama huku pande husika zikiendelea kubadilishana vitisho na mashambulizi katika eneo la Mashariki ya Kati.