1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yasema haina dhamira ya kuunda silaha za nyuklia

25 Septemba 2025

Rais wa Iran Masoud Pezeshkian, ametangaza mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba nchi yake haina dhamira ya kuunda silaha za nyuklia huku zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuanzishwa tena kwa vikwazo.

USA New York 2025 | Rais wa Iran Masoud Peseschkian mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
Rais wa Iran Masoud Pezeshkian akihutubia UNGAPicha: Kyle Mazza/CNP/abaca/picture alliance

Rais wa Iran Masoud Pezeshkian, ametangaza mbele ya hadhara ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba nchi yake haina dhamira ya kutengeneza silaha za nyuklia huku zikiwa zimebaki siku chache kabla ya vikwazo vya kimataifa kuanzishwa tena dhidi ya taifa hilo kutokana na shughuli zake za nyuklia.

"Ninatangaza katika mkutano huu kwamba Iran haijawahi kujaribu, haijaribu na haitojaribu utengenezaji wa silaha za nyuklia," alisema Rais Pezeshkian.

Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimechukua hatua ya kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa ambavyo vilikuwa vimesitishwa chini ya mkataba wa nyuklia wa 2015 ambao ulifikiwa na Marekani na kisha kuvunjwa na Rais wa Marekani Donald Trump. Vikwazo hivyo vinatazamiwa kuanza kutekelezwa siku ya Jumamosi. Waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Araghchi alikutana Jumanne na mawaziri wenzake wa Ulaya, ikionekana kama njia ya kuepusha vikwazo na kuendeleza mazungumzo.

Baraza Kuu la Umoja wa MataifaPicha: Michael M. Santiago/AFP/Getty Images

Rais Pezeshkian amezikosoa juhudi za Uingereza, Ujerumani na Ufaransa kuanzisha utaratibu wa kurejesha vikwazo na kuzuia makubaliano ya dakika za mwisho juu ya kushindwa kwa Iran kuzingatia masharti ya makubaliano ya nyuklia ya 2015 yenye lengo la kuzuia Tehran kutengeneza silaha za nyuklia.

Kiongozi huyo pia alitumia jukwaa hilo kulaani mashambulizi ya Israel na Marekani mnamo mwezi Juni akisema "ni pigo kubwa kwa uaminifu wa kimataifa na matarajio ya amani ya kikanda." Matamshi hayo katika Baraka Kuu la Umoja wa Mataifa ni ya kwanza kuyatoa katika Jukwaa la Kimataifa tangu vita vya siku 12 kati ya Iran na Israel vilivyoshuhudia mauaji ya maafisa waandamizi wa kijeshi na kisiasa wa Tehran.

"Nyote mlishuhudia kuwa mwezi Juni nchi yangu ilikumbwa na mashambulizi ya kinyama, kinyume na kanuni zote za sheria za kimataifa. Mashambulizi ya anga ya utawala wa Kizayuni na Marekani, dhidi ya miji, nyumba na miundombinu ya Iran, wakati tukiwa katika mkondo wa mazungumzo ya kidiplomasia, yalikuwa ni uhaini mkubwa dhidi ya diplomasia, utulivu na amani."

Kiongozi wa Syria naye aionyoshea kidole Israel

Rais mpya wa Syria Ahmed al-Sharaa ameonya kwamba mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel yanaliweka eneo la Mashariki ya Kati hatarini, lakini ameunga mkono diplomasia huku akipata uungwaji mkono katika hotuba yake ya kwanza ya Umoja wa Mataifa. Sharaa ndiye rais wa kwanza wa Syria kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa miongo kadhaa, na hivyo kuashiria mabadiliko ya haraka kwa mpiganaji huyo wa zamani ambaye hadi mwaka jana alikuwa katika darubini za Marekani. Sharaa, mmoja wa viongozi waliofuatiliwa kwa karibu sana katika mkutano huo wa Umoja wa Mataifa, alisema kuwa Syria imefungua ukurasa mpya baada ya utawala wa nusu karne wa familia ya Assad.

Kiongozi wa Syria Ahmad Al-SharaaPicha: Michael M. Santiago/AFP/Getty Images

"Syria imebadilika kutoka nchi ya mgogoro hadi kuwa fursa ya amani," alisema Sharaa katika hotuba yake kwenye mkutano huo. Lakini ameonya kwamba Israel ambayo imekuwa ikimshambulia mara mara hasimu wake wa kihistoria tangu anguko la Assad, inaharibu ustawi wa Syria.

Naye Rais wa Kenya William Ruto, ambaye alituma maafisa wa polisi kuongoza kikosi cha kimataifa nchini Haiti, ameutolea wito Umoja wa Mataifa kutoa rasilimali zaidi ili kuongeza nguvu katika kurejesha utulivu katika taifa hilo lililoharibiwa na ghasia. Ruto alisifu ujumbe huo kwa mafanikio kama vile kufunguliwa tena ikulu ya rais, makao makuu ya polisi na shule, barabara na viwanja vya ndege. Hata hivyo amesema kikosi hicho kinakabiliwa na uhaba wa wafanyakazi na vifaa.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW