Iran yataka uhakikisho wa hatima ya makubaliano ya kinyuklia
16 Mei 2018Haya yanajiri wakati nchi za Ulaya zilizosaini makubaliano kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran zikifanya juhudi kujaribu kuyanusuru.
Iran imesema leo kwamba vikwazo vipya vilivyowekwa dhidi yake na Marekani ni jaribio la kuvuruga juhudi za kuokoa makubaliano ya kinyuklia ya mwaka 2015 zinazofanywa na mataifa yaliyobaki yaliyotia saini kufuatia kujitoa kwa Marekani kutoka mkataba huo.
Wizara ya fedha ya Marekani jana iliweka vikwazo dhidi ya gavana wa benki kuu ya Iran , watu wengine watatu na benki ya nyingine iliyoko Iraq, wiki moja baada ya rais Donald Trump kuiondoa nchi yake kutoka katika makubaliano hayo na Iran yaliyotiwa saini na mataifa yenye nguvu kuzuwia mpango wake wa kinyuklia.
Iran imevieleza vikwazo hivyo kuwa ni kinyume na sheria na imeonya kwamba iwapo mazungumzo ya kuokoa makubaliano hayo yatashindwa, itaanza tena mpango wake wa kinyuklia katika kiwango cha juu zaidi kuliko hapo kabla.
"Kwa hatua hizo za uharibifu , serikali ya Marekani inajaribu kushawishi dhamira na uamuzi wa mataifa mengine yaliyobaki yaliyotia saini makubaliano hayo ya JCPOA," amesema msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Iran Bahram Qasemi akinukuliwa akisema na shirika la habari la Iran Fars.
Mchakato mpya
Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani walikutana mjini Brussels jana kuangalia vipi wanaweza kuokoa makubaliano hayo ya kinyuklia bila Marekani , lakini mataifa hayo yanaonekana kupata mbinyo mkali kuhusiana na vipi makampuni yao yanaweza kuendelea kufanya biashara na Iran mara Marekani itakapoanza kurejesha vikwazo.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Mohammad Javad Zarif alisema mkutano wao ulikuwa mwanzo mzuri, lakini anataka kuona uhakikisho ukifanyakazi.
"Tumeanza mchakato , ambao unahitaji kufanyika kwa nguvu kabisa, na hatuma muda wa kutosha. Tunahitaji kufikia hatua fulani ya uhakika ambao utahakikisha mafanikio kwa Iran katika muda maalum ambao rais alisema wiki chache zilizopita. Tutaona iwapo dhamira ya kisiasa ambayo imeelezwa na washiriki waliobakia katika mkataba huo wa JCPOA unaweza kutafsiriwa katika kufanyakazi."
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema kwamba njia bora ya kushughulikia wasi wasi wa kimataifa juu ya jukumu la Iran katika kanda ya mashariki ya kati pamoja na mpango wake wa makombora ni katika utaratibu wa makubaliano ya kinyuklia, hata iwapo Marekani imejitoa.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Gakuba, Daniel