1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yatakiwa kuchukua hatua kuhusu mpango wa nyuklia

24 Septemba 2025

Ujerumani, Ufaransa, na Uingereza zimeitaka Iran kuchukua hatua madhubuti kushughulikia wasiwasi wa muda mrefu kuhusu mpango wake wa nyuklia, zikitahadharisha kuwa muda unayoyoma.

Rafael Grossi na Jean-Noel Barrot
Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kudhibiti matumizi ya nishati ya nyuklia, IAEA Rafael Grossi na Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Jean-Noel BarrotPicha: Selcuk Acar/Anadolu/picture alliance

Nchi hizo tatu za Ulaya, maarufu kama E3, kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya, zimeitaka Iran kuchukuwa hatua kuhusu mpango wake wa nyuklia, zikitahadharisha kuwa muda wa kufikia suluhu ya kidiplomasia unayoyoma.

Mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa hayo, Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Yvette Cooper, mwenzake wa Ufaransa Jean-Noël Barrot na Johann Wadephul wa Ujerumani, walikutana na mwenzao wa Iran, Abbas Araghchi, pembezoni mwa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, wakisisitiza kuwa Tehran inapaswa kuchukua hatua za haraka na kwa muda mfupi.

Katika taarifa yao kupitia mtandao wa X, mataifa ya E3 yameitaka Iran irejee mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani na kuliruhusu Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, IAEA, kufikia vinu vyote vya nyuklia, kama inavyotakiwa chini ya makubaliano ya kimataifa.

Mataifa hayo pia yalionya kuwa yako tayari kukamilisha mchakato wa kurejesha vikwazo iwapo Iran haitatekeleza wajibu wake, lakini yakasisitiza kuwa juhudi za kidiplomasia zitaendelea hata baada ya vikwazo kuanza kutekelezwa. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema suala la amani katika eneo hili inaweza kupatikana tu ikiwa mpango wa nyuklia wa Iran utatutiliwa.

"Amani katika eneo hili inaweza kupatikana tu ikiwa mpango wa nyuklia wa Iran, ambao umeharibiwa kwa sehemu tu, utakuwa tena chini ya udhibiti kamili. Kwa sababu hiyo, Ufaransa, Ujerumani na Uingereza, kwa makubaliano ya pamoja, zimeanzisha mchakato wa kurejesha vikwazo vyote vya kimataifa vilivyowahi kuiwekea Iran."

Iran imeendelea kusisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni wa kiraia, lakini shirika la IAEA liliripoti kuwa kabla ya vita ya mwezi Juni kati ya Iran na Israel, Tehran ilikuwa na zaidi ya kilo 400 za madini ya urani yaliyorutubishwa kwa kiwango cha asilimia  60 ambacho ni kiwango cha juu zaidi. Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, amekataa mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani kuhusu mpango wa nyuklia, akisema kuwa mazungumzo hayo ni njia isiyo na matumaini.

"Kwa maoni yangu, kufanya mazungumzo na Marekani kuhusu suala la nyuklia, na labda hata kuhusu masuala mengine, ni njia isiyo na matumaini kabisa "

Wakati huo mataifa ya G7, yakiongozwa na Marekani, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, Italia, Japani na Kanada, pia yalitoa wito kwa Iran kutekeleza wajibu wake wa nyuklia, kurejesha ushirikiano na shirika la IAEA na kuanza tena mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani.

Katika taarifa yao, G7 walipongeza hatua ya E3 kuanzisha utaratibu wa makubaliano ya nyuklia ya Iran ya mwaka 2015 wakisema ni hatua stahiki kufuta ukiukaji mkubwa wa makubaliano ya Vienna ya mwaka 2015.

Makubaliano hayo ya Vienna yalilenga kuizuia Iran kutengeneza silaha za nyuklia, na yalionekana kama mafanikio ya kidiplomasia. Katika hotuba yake kwenye Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Rais Trump aliukosoa vikali Umoja huo kwa kushindwa kutatua matatizo ya msingi iliwemo suala la nyuklia ambalo ni tishio linaendelea kwa nchi za Ulaya.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW