1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yatangaza kurutubisha zaidi madini ya Urani

Babu Abdalla5 Novemba 2019

Kwa mara nyingine Iran imetangaza kukiuka makubaliano ya mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 yalioidhinishwa na mataifa yenye nguvu duniani kwa kuunda mitambo ya kurutubisha madini ya Urani kufikia viwango vya 1,044. 

Iran IR 6 Zentrifugen
Picha: picture-alliance/AP Photo/IRIB

Tangazo la kukiuka makubaliano ya mkataba wake wa nyuklia limetolewa siku ya Jumatatu na Rais Hassan Rouhani katika hotuba yake kupitia runinga ya kitaifa.

Katika makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015, Iran inaruhusiwa kuongeza viwango vya kurutubisha madini ya Urani japo bila kuongeza gesi kinyume na tangazo lililotolewa na Rouhani.

Hapo Jumatatu Iran ilizindua mitambo aina ya 30 IR-6 ya kurutubisha madini ya Urani na kwa sasa taifa hilo lina mitambo 60 ya kisasa hali inayoonesha upeo na azma yake.

Mkuu wa shirika la nishati ya Atomiki nchini Iran Ali Akbar Salehi amesema Iran iliyokuwa inazalisha gramu 450 sawa na pauni moja ya madini ya Urani kwa siku, sasa itakuwa inazalisha kilo 5 ambayo ni sawa na pauni 11 kwa siku.

Iran imeiita hatua hiyo kuwa majibu ya moja kwa moja kwa rais wa Marekani Donald Trump kuiondoa Marekani katika makubaliano ya nyuklia yaliyotiwa saini mwaka 2015.

Rais Hassan Rouhani wa Iran Picha: farsnews

Pia uzinduzi wa mitambo hiyo unaonekana kama njia ya kujiimarisha baada ya Marekani kuiwekea vikwazo ambavyo vimekuwa na athari kubwa kwa biashara ya mafuta.

Hata hivyo, Rais Rouhani anasema Iran inaweza kubadilisha uamuzi huo iwapo mataifa yenye nguvu duniani yatatoa suluhu kwa vikwazo walivyowekewa na Marekani ambavyo vimeathiri soko lake la mafuta.

Umoja wa Ulaya umeitolea wito Iran kurudi katika makubaliano ya mkataba wake wa nyuklia.

Kuvunjika kwa makubaliano hayo ya nyuklia kumekuja wakati ambapo kumeshuhudiwa mashambulizi kadhaa dhidi ya visima vya mafuta vya Saudia, huku Marekani ikiilaumu Iran kwa mashambulizi hayo.

Hata hivyo katika hatua ya kushangaza, wakala wa kimataifa ya nishati ambayo ina jukumu la kudhibiti utumizi wa nishati duniani haijasema lolote kuhusu tangazo hilo la Iran.

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW