1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIran

Iran yatishia kujibu vikali mashambulizi yoyote ya Marekani

23 Februari 2026

Iran imesema uvamizi wa kiwango chochote wa Marekani utaifanya Jamhuri hiyo ya Kiislamu kujibu "vikali", baada ya matamshi ya Rais Donald Trump kwamba anafikiria kufanya mashambulizi machache dhidi ya nchi hiyo.

Bahari ya Arabia 2026 | F/A-18E Super Hornet ikijiandaa kupaa kutoka kwa meli ya kubeba ndege ya USS Abraham Lincoln
Marekani imekita majeshi yake kwenye eneo la Mashariki ya Kati kwa lengo la kuiongezea shinikizo Iran ili iingie makubaliano kuhusu mipango yake ya nyukliaPicha: Daniel Kimmelman/US Navy/AFP

Mapema Jumatatu, wizara ya mambo ya nje ya Iran ilirudia tena kusema shambulizi lolote, hata likiwa dogo kiasi gani linaweza kuchukuliwa kama kitendo cha uvamizi na si vinginevyo. Msemaji wa wizara hiyo Esmaeli Baqaei amesema alipozungumza na waandishi wa habari kwamba kama ilivyo kwa taifa jingine, Iran nayo itajibu vikali kitendo cha uchokozi kama sehemu ya haki yake ya kujilinda.

Mataifa hayo mawili yalihitimisha awamu ya pili ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ya mipango ya nyuklia ya Iran, nchini Uswisi Jumanne iliyopita chini ya uratibu wa Oman. Lakini Marekani tayari imepeleka majeshi yake huko Mashariki ya Kati ili kuiongezea shinikizo Iran, ifikie makubaliano katika mazungumzo yanayotarajiwa kufanyika kwa mara nyingine siku ya Alhamisi, huku Trump akizungumzia mashambulizi hayo madogo ikiwa makubaliano hayatafikiwa.

Mazungumzo hayo tayari yamethibitishwa na Iran na Oman, lakini Marekani bado haijathibitisha.

Umoja wa Ulaya wataka suluhu ya kidiplomasia

Umoja wa Ulaya, ambao umetengwa katika mazungumzo ya upatanishi kuhusu Iran, umetoa wito wa suluhu ya kidiplomasia kabla ya mazungumzo hayo. Mkuu wa sera ya kigeni kwenye umoja huo Kaja Kallas alipozungumzia hilo kabla ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni alisema hawako tayari kuona vita vingine kwenye ukanda huo.

"Hali nchini Iran, bila shaka, ni ya mashaka makubwa. Kwa hivyo hatuhitaji vita vingine katika eneo hili. Tayari tumeelemewa. Kwa hivyo tumesisitiza njia ya kidiplomasia ya kusuluhisha hili. Pia tuko tayari kuchangia. Na si suala la nyuklia tu, bali pia mpango wa makombora ya balistiki na wasiwasi mwingine tulionao dhidi ya Iran. Ni kweli kwamba Iran ni dhaifu sana kwa wakati huu kuliko ilivyo kawaida, na tunapaswa kutumia fursa hii kupata suluhisho la kidiplomasia."

Maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu wanaopinga mfumo wa utawala wa kimabavu yameendelea kwa siku ya tatu mfululizo hadi siku ya Jumatatu.Picha: UGC/AFP

Mamlaka za Iran zimekabiliwa na changamoto kubwa hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na wimbi la maandamano makubwa mnamo mwezi Januari, vita vya siku 12 na Israel mwaka jana na kudhoofika kwa ushirikiano na washirika wake wa kikanda.

Mataifa yataka raia wake waondoke Iran

Na huko New Delhi taarifa zinasema wizara ya mambo ya nje ya India imewarai raia wake kuondoka Iran, kufuatia kitisho cha Marekani kulivamia taifa hilo. Ubalozi wa India mjini Tehran umesema kwenye taarifa yake iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba kutokana na hali ya mambo inavyokwenda, raia wa India ambao kwa sasa wako Iran wanashauriwa kuondoka kwa njia yoyote ya usafiri iliyopo ikiwa ni pamoja na ndege za biashara.

Ubalozi wa India unakisia kuna raia kama 10,000 wa India waliomo nchini humo. Ni tahadhari inayotolewa kabla ya ziara inayotarajiwa ya Waziri Mkuu wa India Narendra Modi nchini Israel siku ya Jumatano. Kulingana na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu jana Jumapili, ziara ya Modi itasaidia kujenga ushirika mpya wa kukabiliana na kile alichokieleza kama maadui "wenye msimamo mkali".

Waziri Mkuu wa India anazuru Israel katikati ya mvutano unaoongezeka kati ya Iran na Marekani kuhusu mipango ya Iran ya nyukliaPicha: Gil Cohen-Magen/AFP/Getty Images

Modi naye aliyezuru Israel mara ya mwisho mwaka 2017, alisema jana Jumapili kwamba alikuwa ana matarajio makubwa, baada ya mazungumzo na Modi wakati wa ziara hiyo na kuongeza kuwa India inathamini sana urafiki wa kudumu na Israel, uliojengwa kwa misingi ya uaminifu, uvumbuzi na ushirikiano katika kuleta amani na maendeleo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani nayo imewaamuru wanadiplomasia na familia zisizo na shughuli muhimu kuondoka Lebanon huku mvutano na Iran ukiongezeka.

Na huko mjini Tehran, maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu wanaopinga mfumo wa utawala wa kimabavu yameendelea kwa siku ya tatu mfululizo hadi leo Jumatatu. Hata wanafunzi wa kike walioko kwenye vyuo vinavyopokea wanawake tu pia walishiriki maandamanao hayo, wanaharakati wa Iran walichapisha kwenye mtandao wa Telegram, huku vidio zikionyesha namna wanavyoupinga utawala huo.

Siku ya Jumamosi, vyuo vingi vya Iran vilianza muhula mpya, lakini vikiwa vimechelewa kwa zaidi ya mwezi mmoja. Vyuo vikuu hapo awali vilikuwa vimesimamisha shughuli zao kufuatia maandamano makubwa mapema Januari.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW