1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yatishia kujiondoa mkataba wa nyuklia

4 Mei 2018

Iran imetishia kujiondoa kwenye mkataba muhimu wa nyuklia, iwapo Rais Donald Trump wa Marekani ataamua kuiondoa Marekani kwenye mkataba huo na kuikosoa Ulaya ikidai inamuunga mkono Trump.

Javad Zarif Brüssel Belgien
Picha: Getty Images/J.Thys

Iran imetishia kujiondoa kwenye mkataba muhimu wa nyuklia, iwapo Rais Donald Trump wa Marekani ataamua kuiondoa Marekani kwenye mkataba huo, huku pia ikiyakosoa mataifa ya Ulaya kwa madai kuwa yakubaliana na hatua hiyo ya Marekani. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif, alisema hapo jana kwamba madai yanayotolewa na Rais Donald Trump yanayolenga kuubadilisha mkataba huo uliofikiwa na mataifa saba yenye nguvu zaidi duniani, hayakubaliki, katika wakati ambapo tarehe ya mwisho iliyowekwa na Trump ya kufanya maamuzi hayo ikikaribia.

Zarif amesema kupitia vidio iliyooneshwa kwenye mtandao wa kijamii wa YouTube kwamba Iran haitaingia tena kwenye mazungumzo mapya kuhusu yale waliyokubaliana miaka kadhaa iliyopita na ambayo yamekuwa yakitekelezwa:

Hata hivyo, ukiwacha Marekani, mataifa mengine yaliyosaini mkataba huo wa nyuklia na Iran yamekuwa wakijaribu kumsihi Trump kuuokoa mkataba huo, wakidai kwamba Iran imekuwa ikikubaliana na masharti yake.

Rais Donald Trump wa Marekani ameitaka Ulaya kuurekebisha mkataba huo wa nyuklia wa Iran ili asijiondoe.Picha: picture-alliance/RS/MPI/Capital Pictures/M. Theiler

Trump amesema kama mataifa ya Ulaya hayatarekebisha mapungufu makubwa yaliyomo kwenye mkataba huo wa Iran hadi ifikapo Mei 12, ni dhahiri kuwa atakataa kuongeza nafuu ya vikwazo vya Marekani dhidi ya taifa hilo lenye utajiri wa mafuta.

Trump ameeleza kwamba mkataba huo, ambao Iran ilikubali kudhibiti shughuli zake za kinyuklia, ili badala yake ipatiwe nafuu ya vikwazo vya kiuchumi ni mkataba mbaya zaidi kuwahi kufikiwa.

Iran yasema haitakuwa na namna zaidi ya kujiondoa kwenye mkataba huo iwapo utapitiwa upya.

Kwenye ujumbe wake huo kupitia mtandao wa YouTube, ambayo waziri huyo wa mambo ya nje ya Iran amezungumza kwa lugha ya Kiingereza, amesisitiza kwamba Marekani mara kadhaa imeukiuka mkataba huo wa nyuklia, na hususan kwa kuwanyanyasa wengine kwa kuwazuia kurejesha biashara zao Iran, na kutaka kufikiwa hatua ambapo Marekani itakubaliana na mkataba huo:

Mshauri mwandamizi wa kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Khamenei, pia ameonya kuhusu mataifa ya Ulaya kuhusu kile alichosema ni kuupitia upya mkataba huo wa nyuklia. Amesema washirika wa Marekani, hususan mataifa hayo ya Ulaya yanajaribu kuupitia upya, na moja ya hatua watakayochukua kutokana na mkakati hu itakuwa ni kujiondoa kwenye mkataba huo. 

Mataifa hayo ya Ulaya yaliyosaini mkataba huo yamekuwa yakimsihi rais Trump kusalia kwenye mkataba huo, uliofikiwa na mtangulizi wake Barack Obama.

Zarif, amenukuliwa akisema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, walielezwa kwamba Trump hakuridhika na mkataba huo, lakini sasa inaonekana dhahiri kama mataifa hayo yanamuunga mkono Trump kutokana na namna baadhi ya mataifa hayo yanavyofanya makubaliano na Trump kuhusiana na mkataba huo.

Zarif alikuwa akiijibu Uingereza, Ufaransa na Ujerumani ambao Jumapili iliyopita walisema kwamba baadhi ya masuala muhimu hayakuingizwa kwenye mkataba huo.

Rais  Emmanuel Macron wa Ufaransa alisisitizia kauli yake mnamo siku ya Jumatano kuhusu mkataba huo, lakini akikiri kwamba unahitaji kuimarishwa.

Mwandishi: Lilian Mtono/RTRE/APE/AFPE

Mhariri: Mohammed Khelef