Iran kushambulia vyuo vikuu vya Marekani Mashariki ya Kati
29 Machi 2026
Shirika la habari la Fars, ambalo lina uhusiano wa karibu na Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC), limeripoti kwamba Iran imetishia kuvishambulia vyuo vikuu vya Marekani na mshirika wake Israel katika eneo la Mashariki ya Kati.
Shirika hilo la habari limenukuu taarifa ya kikosi hicho maalum cha walinzi inayosema, ikiwa serikali ya Marekani inataka vyuo vyake vikuu katika eneo hilo viepukane na hatua za kulipiza kisasi, basi ni lazima Marekani ilaani mashambulio ya mabomu yaliyolenga vyuo vikuu vya Iran.
IRGC imewataka Wafanyakazi wote, maprofesa na wanafunzi wa vyuo vikuu vya Marekani katika eneo hilo, pamoja na wakazi wanaoishi kwenye maeneo ya jirani na vyuo hivyo, waondoke na kwenda umbali wa angalau kilomita moja kutoka kwenye vyuo vikuu hivyo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, amesema, Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Isfahan na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia jijini Tehran ni vyuo vikuu viwili kati ya vyuo vikuu vingi na vituo vya utafiti vilivyoshambuliwa kimakusudi katika siku 30 zilizopita za vita vya Israel na Marekani dhidi ya taifa la Iran.
Baqaei ameongeza kusema: "uchokozi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran unaendelea kufichua malengo yao ya kweli ambayo ni kudhoofisha msingi wa kisayansi wa Iran na urithi wa kitamaduni kwa kuvilenga vyuo vikuu, vituo vya utafiti, masanamu ya kihistoria na kwa kuwaua wanasayansi mashuhuri."
Israel na Marekani zilianza mashambulizi yaliyoratibiwa dhidi ya Iran mnamo Februari 28 wakati wa mazungumzo ya kupunguza uwezo wa nchi hiyo kutengeneza silaha za nyuklia. Iran imekuwa ikisisitiza kila mara kwamba mpango wake wa nyuklia ni wa amani tu.
Wiki kadhaa za mashambulio zimesababisha uharibifu mkubwa na vifo nchini humo, wakati ambapo raia wa Iran bado wanakabiliana na athari za msako mkali wa serikali dhidi ya waandamano yaliyofanyika mapema mwaka huu.
Katika hatua za kulipiza kisasi kutokana na vita vya Israel na Marekani, Iran imeufunga Mlango- Bahari wa Hormuz, ambao ni njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta na gesi duniani. Iran pia inaelekeza mashambulizi nchini Israel pamoja na nchi za Ghuba zinazoshirikiana na Marekani.
Walinzi wa Mapinduzi ya Iranwamesema mwishoni mwa wiki walishambulia kwa makombora na ndege zisizo na rubani mitambo ya Aluminium huko Bahrain na katika Umoja wa Falme za Kiarabu, wakielezea kuwa viwanda hivyo vinahusishwa na jeshi la Marekani.
Bahrain na nchi zingine za Ghuba zimekuwa zikilengwa mara kwa mara na makombora na ndege zisizo na rubani za Iran. IRGC imesema mashambulizi hayo ni ya kulipiza kisasi kwa mashambulio ya makombora ya Marekani na Israel dhidi ya miundombinu ya viwanda vya Iran yaliyorushwa kutoka kwenye kambi za kijeshi za Marekani zilizopo kwenye nchi za Ghuba.