Iran yatoa hukumu ya kifo kwa waandamanaji
17 Novemba 2022Tovuti ya mahakama ya mapinduzi nchini Iran inayosikiliza kesi za masuala ya usalama imesema mshtakiwa wa kwanza ametiwa hatiani kwa kumgonga kwa gari lake na kumuua afisa wa polisi, wa pili kwa kumiliki bunduki na kumchoma kisu afisa wa usalama na wa tatu alitiwa hatiani kwa kuzuia magari barabarani na kueneza ugaidi.
Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadamu lenye makao yake nchini Norway IHR Mahmood Amiry-Moghaddam amelaani vikali hukumu hizo za kifo, na kutahadharisha juu ya uwezekano wa watu wengine kunyongwa. Iran hata hivyo inayashtumu mataifa ya Magharibi kwa kuchochea ghasia hizo.
Soma pia: Wanafunzi Iran, wafanyakazi wakaidi ukandamizaji wa maandamano
Shirika la ujasusi la Uingereza M16 limesema jana kuwa Iran inataka kuwateka nyara au kuwaua raia wa Uingereza ambao inawaona kama "maadui wa serikali" na kwamba matukio kama 10 ya njama dhidi ya raia hao yamefichuliwa.
Maandamano ya kuipinga serikali yameingia mwezi wake wa tatu
Ghasia za mitaani ambazo zimeenea kote nchini humo zimezochochewa na kifo cha Mahsa Amini mnamo Septemba 16. Amini, binti mwenye umri wa miaka 22 mwenye asili ya Kikurdi, alifariki akiwa chini ya ulinzi wa polisi wa maadili baada ya kukamatwa kwa madai ya kukiuka kanuni ya mavazi ya wanawake wa Iran.
Kwa mujibu wa video iliyochapishwa mtandaoni na mtandao maarufu unaofuatilia matukio ya siasa na maandamano nchini Iran wa 1500 Tasvir, waandamanaji walisikika wakiimbia kwenye barabara za mji mkuu Tehran "Tutapigana! Tutakufa! Tutaichukua Iran!"
Video nyengine iliyothibitishwa na shirika la habari la AFP, imeonyesha vikosi vya usalama, wakiwemo polisi waliovalia mavazi ya raia, wakiwashambulia wanawake wasiokuwa na vazi la hijabu kwenye treni ya chini ya ardhi.
Soma pia:Polisi Iran yaendeleza ukandamizaji wa maandamano
Takriban watu saba wameripotiwa kupoteza maisha yao kufuatia ghasia hizo ndani ya muda wa siku mbili.
Idadi hiyo ya wahanga haikujumuisha watu watano ambao mamlaka inasema waliuawa na watu wenye silaha waliowashambulia waandamanaji na polisi jana Jumatano katika mkoa wa kusini magharibi wa Khuzestan.
Vyombo vya habari vya serikali vimesema, "waeneza ghasia"- neno linalotumiwa na maafisa kuwaelezea waandamanaji- wamewaua wanachama wawili wa jeshi la walinzi wa mapinduzi na mwanachama mmoja wa kikosi cha jeshi la Basij siku ya Jumanne.
Mamlaka inajitahidi kadri iwezavyo kuzima maandamano hayo kwa kutumia nguvu na kuendesha kampeni ya kamata kamata ya wanaharakati, waandishi wa habari na wanasheria. Lakini licha ya hayo, maandamano hayo hayajaonyesha dalili ya kupungua.
Aghalabu mamlaka imekuwa ikizima mtandao wa intaneti na kufanya iwe vigumu kuthibitisha ripoti za ghasia zinazoripotiwa katika maeneo mengine ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu.