Iran yatumai kurejesha mahusiano na Saudi Arabia
13 Januari 2023Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran Amir-Abdollahian ameelezea matumaini yake kuwa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tehran na Riyadh yanaweza kurejeshwa kupitia mazungumzo kati ya mahasimu hao wawili wa kikanda. Saudi Arabia ilivunja mahusiano na Iran Januari 2016, baada ya ubalozi wake mjini Tehran na ubalozi mdogo wa mji wa pili, Mashhad, kushambuliwa na waandamanaji kufuatia hatua ya Riyadh kumnyonga mhubiri wa Kishia, Nimr al-Nimr.
Akizungumza hivi leo wakati wa ziara yake nchini Lebanon, Amir-Abdollahian amesema anatumai ofisi za ubalozi mjini Tehran na Riyadh zitafunguliwa tena katika mkakati wa mazungumzo ambayo yanapaswa kuendelea kati ya nchi hizo mbili. Tangu Aprili 2021, Iraq imeandaa msururu wa mikutano kati ya pande hizo mbili lakini mazungumzo hayo yamekwama katika miezi ya karibuni.