Iran yaufunga Mlango Bahari wa Hormuz
18 Februari 2026
Tangu Marekani kuanzisha vitisho vya kuishambulia Iran, hii ni mara ya kwanza kwa Tehran kutangaza kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz ambayo ni njia muhimu ya kimataifa inayotumiwa kusafirisha asilimia 20 ya mafuta yanayotumiwa kote duniani.
Wakati Marekani ikiongeza uwepo wa vikosi vyake vya kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati, Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ameonya kwamba hata jeshi lenye nguvu zaidi duniani linaweza wakati mwingine kupata pigo kubwa kiasi cha kushindwa kusimama tena.
Wakati mazungumzo yalipoanza, vyombo vya habari vya Iran vilitangaza kuwa wanajeshi wa Iran walifyatua makombora kuelekea ujia huo wa bahari na kwamba wataufunga kwa saa kadhaa kwa ajili ya kile walisema ni „wasiwasi wa usalama na shughuli za baharini".
Mwanadiplomasia wa Iran aona fursa kwenye mazungumzo
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Araghchi baadaye alionyesha mtazamo tofauti, akielezea matumaini kuhusu mazungumzo hayo na kusema "dirisha jipya limefunguka" kwa ajili ya kufikia makubaliano. Abbas aliyasema hayo katika Kongamano la Umoja wa Mataifa la Unyang'anyaji Silaha baada ya kuongoza ujumbe wa Iran katika mazungumzo yaliyofanyika Geneva. "Tuna matumaini kwamba mazungumzo yataleta suluhisho endelevu na ambalo linaweza kutosheleza maslahi ya pande husika na kanda nzima. Wakati huo huo, kama ilivyoonyeshwa wakati wa shambulizi la tarehe 13 Juni 2025, Iran inaendelea kuwa tayari kikamilifu kujilinda dhidi ya tishio au kitendo chochote cha uchokozi. Matokeo ya shambulio lolote dhidi ya Iran hayataishia mipakani mwake." Alisema Abbas.
Hakutaja waziwazi mazoezi ya kijeshi au kufungwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz.
Rais wa Marekani Donald Trump, ambaye alifuta makubaliano ya awali ya nyuklia na Iran wakati wa muhula wake wa kwanza, ametishia mara kwa mara kutumia nguvu kuilazimisha Iran kukubali kuzuia mpango wake wa nyuklia. Iran imesema itajibu kwa kufanya shambulio. Trump pia ameitishia Iran kuhusu mauaji ya waandamanaji.
Vance asema mazungumzo yalienda vizuri
Wajumbe wa Trump, Steve Witkoff na Jared Kushner, waliongoza ujumbe wa Marekani katika mazungumzo ya hivi karibuni yasiyo ya moja kwa moja, yaliyofanyika ndani ya makazi ya mjumbe wa Oman huko Geneva.
Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance alisema katika mahojiano na Fox News Channel baada ya kuzungumza na Witkoff na Kushner, kuwa "Kwa njia fulani, mambo yalikwenda vizuri, "Lakini kwa njia nyingine, ilikuwa wazi kabisa kwamba rais ameweka mistari nyekundu ambayo Wairan bado hawajakubali kuitambua na kuifanyia kazi." Alisema.
Vyanzo: Mashirika