Iran yaitetea nafasi yake katika siasa za Mashariki ya kati
20 Januari 2017Ushindi wa majeshi ya Syria mwezi uliopita baada ya kuuteka mji wa mashariki mwa Aleppo ambao ulikuwa ngome ya waasi umeitumbuza Iran katikati mwa mvutano wa kidiplomasia unaoendelea kuhusu mustakabali wa baadaye wa taifa hilo. Ushindi huo ulitokana na msaada muhimu kutoka kwa washauri wa jeshi la Iran na maelfu ya wapiganaji wa kujitolea. Rais Hassan Rouhani alisema wiki hii kuwa waandaaji wa mazungumzo hayo ya amani yatakayoanza mjini Astana, Jumatatu wiki ijayo, ambao ni Iran, Urusi na Uturuki, ndio mataifa pekee yenye ushawishi wa kusitisha uhasama kati ya serikali ya Syria na waasi ili kupatikana amani ya kudumu.Lakini kuyashughulia maslahi ya kila mdhamini wa mazungumzo hayo ndicho kuzungumkuti.
Iran, mshirika mkubwa wa Rais Bashar al-Assad, inataka kupewa kipaumbele hakikisho la kusalia madarakani kwa Assad au angalau mpangilio kwa kuaminika wa serikali ya mpito, kuhakikisha Syria haitumbukii katika mikono ya watu wenye misimamo mikali, au serikali inayounga mkono wapinzani wa Rais Assad, yaani mataifa ya Saudi Arabia na Marekani. Iran pia inataka kudumisha njia salama kwenda Lebanon kupitia Iraq na Syria, ambapo washirika wake wa Hizbullah wamekuwa wakizozana kwa muda mrefu na Israel. "Vita vya Syria havionekani kuwa vya wenyewe kwa wenyewe nchini Iran, badala yake vinachukuliwa kuwa vita vya kuamua siasa za Mashariki ya Kati," anasema Adhan Tabatabai - mchambuzi kutoka Iran na mkurugenzi mtendaji na shirika la CARPO lenye makao yake nchini Ujerumani.
Serikali ya Tehran inaamini kuwa Israel ingelifanya mashambulizi ya angani dhidi ya vinu vya nyuklia vya Iran iwapo Hizbullah haingekuwepo kama kuzuizi katika mpaka wa Israel na Lebanon, anasema Tabatabai.
Mazungumzo kati ya Iran na Uturuki, ambayo inayaunga mkono makundi ya waasi nchini Syria, daima yatasalia kuwa mwiba. Kinachoshangaza zaidi ni mipasuko iliyoanza kujitokeza katika mahusiano kati ya Iran na Urusi, ambayo imekuwa msadizi mkubwa wa Rais Assad. Iran ina wasiwasi kuwa Urusi inaonekana kuegemea upande wa Uturuki kwa kushirikiana na vikosi vya Uturuki kukabiliana na kundi lijiitalo Dola la Kiislamu (IS) na pia kuitenga Iran katika mazungumzo ya awali ya kusitisha mapigano kaskazini mwa Syria.
Hata hivyo, Iran inaweza kujivunia kuhusu mafanikio kadhaa katika eneo la Mashariki ya Kati katika miezi ya hivi karibuni, kuanzia vita vya Syria hadi kuchaguliwa mgombea wa urais iliyekuwa ikimuunga mkono nchini Lebanon.
Kujumuishwa katika meza ya mazungumzo ya amani kuhusu Syria ni hatua muhimu kwa Iran, ambayo ilikuwa imezuiwa katika mazungumzo ya awali yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa. Makubaliano juu ya mpango wa nyuklia iliyoyatia saini 2015 na mataifa yenye nguvu duniani yaliirejesha kuwa imara na kuisaidia kupata nafasi katika mkutano wa kimataifa kuhusu Syria mjini Vienna mwezi Oktoba mwaka huo wa 2014.
Wakati huo ilikuwa vigumu kupuuza jukumu muhimu la Iran katika mapigano ya Syria. Iran hutoa maelezo machache kuhusu ushiriki wake nchini Syria, lakini mwezi Novemba ilifichua kuwa zaidi ya wapigaji 1,000 wa kujitolea walikuwa wameuawa nchini Syria, wengi wao wakiwa ni wale waliosajiliwa kutoka jamii za Kishia nchini Afghanistan na Pakistan.
Mwandishi: Jane Nyingi/AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef