1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yazidisha vitisho licha ya kutaka muafaka na Marekani

6 Mei 2025

Iran inatoa kauli kali - huku bado ikitaka kuendelea na mazungumzo zaidi na Marekani kuhusu uwezekano wa kufikia makubaliano ya nyuklia. Hata hivyo, imesisitiza kuwa haitakubali masharti mapya yanayokiuka misimamo yake.

Iran Teheran 2025 | Jalada la gazeti kuhusu mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na Marekani mjini Roma likiwa kwenye kibanda cha magazeti.
Mazungumzo ya matumaini na mashaka: Marekani na Iran wanajadili hatma ya makubaliano ya nyuklia Picha: Atta Kenare/AFP/Getty Images

Katika siku za hivi karibuni,Iran imeunga mkono shambulio lililofanywa na waasi wa Houthi kutoka Yemen, ambalo lilipenya mfumo wa ulinzi wa makombora wa Israel na kulenga karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Ben-Gurion. Iran pia ilionesha picha za jaribio la kombora lake la masafa marefu, huku Waziri wa Ulinzi wa Iran akijibu vitisho vilivyotolewa na Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth.

Shirika moja linalohusiana na Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi cha Iran (Revolutionary Guard) pia lilizindua mchoro mpya wa ukutani unaoonyesha ramani ya Israel iliyofunikwa na alama za malengo ya makombora, yaliyopangwa kwa umbo la jambiyya, kisu cha jadi cha Yemen.

Hata hivyo, licha ya msimamo huu mkali, Iran inasisitiza kuwa bado inataka kufikia makubaliano ya nyuklia na Marekani. Mazungumzo yaliyopangwa kufanyika wikiendi iliyopita mjini Rome hayakufanyika. Wakati huo huo, maafisa wa utawala wa Trump wanaendelea kushikilia kuwa Iran inapaswa kuacha kabisa uwezo wake wa kurutubisha urani ili vikwazo vya kiuchumi viondolewe — jambo ambalo Iran imepinga waziwazi mara kadhaa.

 Mvutano mpya kufuatia vita vya Israel na Hamas

Msimamo huu wa Iran unaonekana kuwa wa mkanganyiko, lakini ndio hali halisi ambayo Tehran inajikuta ndani yake. Hii ni baada ya muda mrefu wa kuwa na ushawishi mkubwa katika Mashariki ya Kati kupitia kile inachokiita "Mhimili wa Upinzani” — yaani, mataifa na makundi yenye msimamo mkali yanayoungana dhidi ya Israel na Marekani.

Mvutano kati ya Iran na Marekani na washirika uliongezeka baada ya shambulizi la Wahouthi dhidi ya uwanja wa ndege wa Ben Gurion, Mei 4, 2025.Picha: Chen Junqing/Xinhua/picture alliance

Lakini hali ilibadilika baada ya shambulio la kundi la Hamas dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7, 2023, ambapo watu wapatao 1,200 waliuawa na wengine 250 kuchukuliwa mateka na kupelekwa Ukanda wa Gaza. Israel ilijibu kwa kuanzisha vita vikali dhidi ya Hamas, ambavyo vinaendelea hadi sasa — na huenda vikazidi baada ya Israel kuidhinisha mpango wa kuuteka kabisa Ukanda wa Gaza na kubaki huko kwa muda usiojulikana.

Soma pia: Netanyahu: Tutalipa kisasi dhidi ya Wahouthi

Vita hivyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 52,000 huko Gaza, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, kulingana na maafisa wa afya wa Palestina ambao hawatofautishi kati ya raia na wapiganaji katika takwimu zao.

Katika muktadha wa vita hivyo, Hamas, Hezbollah kutoka Lebanon, na makundi mengine yanayoungwa mkono na Iran yamekumbwa na mashambulizi makali ya Israel. Rais wa Syria, Bashar al-Assad — mshirika wa muda mrefu wa Iran — aliondolewa madarakani mwezi Desemba baada ya waasi kuikomboa nchi hiyo.

Hii imeiacha Iran ikiwa na mshirika mmoja wa karibu — waasi wa Kihouthi nchini Yemen — ingawa nao sasa wanakabiliwa na kampeni mpya ya mashambulizi kutoka kwa Marekani chini ya utawala wa Trump.

Iran yaunga mkono kwa tahadhari shambulio la Wahouthi dhidi ya Israel

Shambulio la Jumapili dhidi ya uwanja wa ndege wa Ben-Gurion limepewa uzito mkubwa na vyombo vya habari vya serikali ya Iran. Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ilisisitiza kuwa shambulio hilo lilikuwa "uamuzi wa kujitegemea” uliochukuliwa na kundi hilo.

Wataalamu wanatofautiana kuhusu kiwango halisi cha ushawishi wa Iran kwa waasi wa Houthi. Hata hivyo, Tehran imekuwa na mchango mkubwa katika kuwapatia silaha waasi hao katika vita vya Yemen vinavyoendelea kwa zaidi ya muongo mmoja, licha ya vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa.

Israel yadaiwa kuishambulia Iran

01:17

This browser does not support the video element.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, alisema Jumatatu kwamba, "Watu wa Yemen, kwa hisia zao za kibinadamu na mshikamano wa kidini na Wapalestina, na pia kujilinda dhidi ya mashambulizi ya mara kwa mara ya Marekani, wamechukua hatua fulani.”

Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Iran, Jenerali Aziz Nasirzadeh, alimjibu Waziri mpya wa Ulinzi wa Marekani aliyekuwa ameonya kuwa Iran italipa gharama kwa kuwapatia Houthi silaha.

"Nashauri maafisa wa Marekani wanaotoa vitisho, hasa Waziri mpya wa Ulinzi, wasome historia ya Iran katika miongo minne iliyopita,” alisema Jenerali huyo. "Wakisoma, watagundua kuwa hawapaswi kuzungumza na Iran kwa lugha ya vitisho.”

Soma pia:Trump atangaza mazungumzo ya moja kwa moja ya nyuklia na Iran 

Hata hivyo, hadi sasa Iran haijajibu mashambulizi ya angani ya Israel yaliyoilenga miundombinu yake ya ulinzi wa anga na mpango wa makombora mnamo Oktoba.

Makubaliano ya nyuklia bado ni kipaumbele kwa Iran

Licha ya mvutano huo, kufikia makubaliano mapya ya nyuklia na Marekani bado ni kipaumbele kwa Iran. Mkataba huo unaweza kuishinikiza Tehran kupunguza kiwango cha urutubishaji wa urani na hifadhi yake, kwa matumaini ya kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi. Sarafu ya Iran, rial, ambayo ilikuwa inabadilishwa kwa zaidi ya milioni moja kwa dola moja, imetengemaa na kufikia 840,000 kwa dola moja kutokana na matumaini ya mazungumzo hayo pekee.

Hata hivyo, bado kuna mwanya mkubwa kati ya pande hizo mbili. Vyombo vya habari vya Iran viliripoti kwamba Rais Donald Trump aliweka muda wa mwisho wa miezi miwili kwa Iran katika barua aliyoituma kwa Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei, mnamo Machi 5, kupitia mwanadiplomasia wa Umoja wa Falme za Kiarabu mnamo Machi 12.

Wakati huo huo, kampeni ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Yemen na ongezeko la mashambulizi ya Israel huko Gaza vinaendelea kuibana Tehran.

Israel yaishutumu Iran kuhusu nyuklia

00:48

This browser does not support the video element.

Hii inajumuisha vitisho vya maafisa wa Marekani, wakiwemo Trump mwenyewe, vya kuiwekea vikwazo yoyote itakayoinunua mafuta ghafi ya Iran, sambamba na msimamo mkali unaotaka Iran isipate tena uwezo wa kurutubisha urani hata kidogo. Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ambaye aliwahimiza Trump kujiondoa kwenye mkataba wa awali wa nyuklia mwaka 2018, pia anasukuma ajenda hiyo hiyo kwa nguvu.

Iran inaaminika kuwa inajaribu kuwasilisha ujumbe kwa Marekani licha ya kuahirishwa kwa mazungumzo yaliyopangwa kufanyika Rome wiki iliyopita. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alisafiri kwenda Islamabad kukutana na Waziri mwenzake wa Pakistan, Ishaq Dar. Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan ilithibitisha kuwa walijadili mazungumzo ya nyuklia.

Araghchi alipokelewa kwa baridi zaidi na Kaja Kallas, mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya. Huku mataifa ya Ulaya yakiwa na uhusiano wa karibu na Iran hapo awali, hatua ya Tehran kuiuzia silaha Urusi kwa ajili ya vita dhidi ya Ukraine imewakera wengi barani humo.

"Niliitaka Iran kusitisha msaada wa kijeshi kwa Urusi na kuonyesha wasiwasi wetu kuhusu raia wa EU wanaoshikiliwa na masuala ya haki za binadamu," Kallas aliandika Jumatatu kupitia jukwaa la X. "Uhusiano wa EU na Iran unategemea maendeleo katika maeneo yote haya."