Iran yazindua makombora ya chini ya ardhini
29 Julai 2020Tukio hilo ambalo limeripotiwa leo na kituo cha televisheni kinachomilikiwa na serikali ya Iran, ndiyo luteka ya hivi karibuni ambayo ilisababisha kambi mbili za kijeshi za Marekani kuchukua tahadhari ya muda.
Kulingana na ripoti ya kituo hicho cha televisheni, ndege zinazoendeshwa bila ya rubani ziliilenga meli hiyo bandia kwa mashambulizi. Lakini haikuonyesha moja kwa moja picha kuhusu uzinduzi wa makombora hayo au ya mashambulizi kwa njia ya ndege hizo zisizohitaji rubani wakati wa mazoezi ya kijeshi. Hata hivyo ujumbe uliokuwa ukiwasilishwa kupitia luteka hiyo uliilenga Marekani.
Mnamo usiku, shirika la habari ambalo si rasmi lakini ambalo lina mafungamano na kikosi hicho cha walinzi wa mapinduzi, kilichapisha picha bandia inayoonyesha meli ya kivita ya Marekani ikiwa katika umbo la jeneza na ikiwa na maneno yaliyomnukuu Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, akiahidi kulipiza kisasi dhidi ya Marekani kwa kumuua aliyekuwa Jenerali Mkuu wa Iran mnamo mwezi Januari.
Kitisho cha mzozo wa kijeshi kati ya Iran na Marekani
Luteka hiyo pamoja na jibu la Marekani kuchukua tahadhari dhidi yake, zinaonyesha kitisho kilichoko cha mgogoro wa kijeshi kati ya Marekani na Iran, baada ya misururu ya matukio ya mwaka uliopita yaliyosababisha Marekani kufanya shambulizi kwa njia ya ndege zinazoendeshwa bila marubani mnamo Januari mwaka huu. Iran ililijibu shambulizi hilo kwa kufyatua makombora na kuwajeruhi wanajeshi kadhaa wa Marekani nchini Iraq.
Japo janga la corona limeziathiri Marekani na Iran kwa miezi kadhaa, kumekuwepo na ongezeko la mvutano kati ya nchi hizo mbili, huku Marekani ikilenga kurefusha vikwazo dhidi ya Iran kuhusu silaha, vilivyotolewa na Umoja wa Mataifa lakini ambavyo vinatarajiwa kufikia mwisho wake mwezi Oktoba.
Kisa cha hivi karibuni nchini Syria kuhusu ndege ya kivita ya Marekani iliyoikaribia ndege ya kubeba abiria ya Iran, pia kimefufua mzozo kati ya nchi hizo.
Soma pia Marekani yaishtumu Iran kwa kukaidi azimio la Umoja wa Mataifa
Makomando wa Iran waonyesha mbinu zao
Sawa na picha ya kanda ya video iliyotangazwa Jumanne, makomando wa jeshi la Iran walionekana wakishuka kwa kamba kutoka katika helikopta kwenye luteka iliyoitwa Nabii Mkubwa wa 14 'Great Prophet 14'. Zana za kulipua ndege pia zilionekana zikifyatua risasi kuilenga ndege aina ya drone karibu na mji wa bandari wa Bandar Abbas.
Kituo cha televisheni kinachomilikiwa na serikali kilionyesha kanda ya video ya makombora yakifyatuliwa kutoka kwenye boti, malori na helikopta. Huku mengine yakilenga meli bandia ya kubeba na kusafirisha ndege.
Kamanda mmoja amesema kuwa kikosi hicho cha Walinzi wa Mapinduzi ambacho hutoa tu maelezo kwa Khamenei pekee, kilipanga pia kufyatua makombora ya masafa marefu wakati wa luteka yao ambayo imeendelea hadi Jumatano.
Unaweza pia kusoma Urusi yatetea uzinduzi wa satelaiti wa Iran
Makombora yaliyofyatuliwa yalisababisha jeshi la angani la Marekani katika kambi ya Al-Dhafra mjini Abu Dhabi kukaa katika hali ya tahadhari, sawa na wenzao katika kambi ya Al-Udeid. Wanajeshi hao walikaa katika hali ya kivita wakati wa luteka hiyo. Hayo yamesemwa na wizara ya Ulinzi.
Video zaidi zilizotangazwa na kituo hicho cha televisheni zilionyesha boti za mwendo kasi zikiizunguka hiyo meli bandia, huku makomando wa Iran. wakionyesha mbinu za namna ya kuwashinda nguvu makomando wa Marekani.
Afisa wa jeshi la Marekani Meja Beth Riordan ambaye pia ni msemaji wa Kamandi kuu ya Marekani katika Umoja wa Falme za Kiarabu amesema tukio hilo lilidumu kwa dakika chache, kabla ya kutangazwa kuwa hakuna kitisho.
(APE)