Iran yazishambulia meli nyengine Hormuz
31 Julai 2026
Kwenye taarifa yake jioni ya Ijumaa (Julai 31), IRGC ilizitaja meli hizo mbili za mafuta kama "zisizoheshimu utaratibu" na kwamba zilishambuliwa na kusimamishwa "huku nyengine nne zikilazimika kubadilisha njia na kurejea zililokuwa."
Jeshi hilo liliongeza kuwa meli hizo zilikuwa zikijaribu kuuvuuka Mlango Bahari wa Hormuz kupitia "njia isiyoruhusiwa", likimaanisha njia iliyoanzishwa na jeshi la Marekani kama mbadala wa ile inayosimamiwa na Tehran kwenye Mlango Bahari huo wa kimkakati panapohusika biashara ya mafuta ulimwenguni.
Iran imekuwa ikiudhibiti kiukamilifu Mlango Bahari huo tangu Marekani na Israel zilipoanzisha vita vyake vya uchokozi mnamo tarehe 28 Februari, ambapo imekuwa ikizitaka meli zote kupata kwanza kibali chake na kulipia tozo maalum ili kuweza kutumia njia hiyo.
Kabla ya vita hivi kuanza, Iran ilikuwa daima imeuacha wazi Mlango Bahari huo na haikuwahi kutoa madai yoyote ya kiusalama ama kiuchumi kwa meli zinazopita.
Siku ya Alkhamis (Julai 30), IRGC ilisema kuwa meli nyengine mbili za mafuta zilizokuwa zikijaribu kupita kwenye Mlango Bahari wa Hormuz zililazimika kurudi zilikotoka, baada ya kushuhudia meli nyengine moja ikiteketea kwa moto.
Baadaye ilifahamika kuwa meli hiyo ilikuwa imepita juu ya mabomu yaliyotegwa baharini na jeshi hilo la Iran.
Kuwait yashambuliwa tena
Jeshi la Kuwait lilisema kwamba lilizitambuwa droni zilizokuwa zikiruka kwenye anga la nchi hiyo Ijumaa alfajiri na kuzidunguwa.
"Uchokozi wa kikatili wa Iran ulilenga maeneo kadhaa yenye mundombinu muhimu na vituo vya kijeshi, ambapo mabaki ya droni zilizodunguliwa yameleta madhara kwa majengo lakini hayakusababisha kifo chochote kile." Ilisema taarifa iliyotumwa mtandaoni na jeshi hilo.
Kuwait na mataifa mengine ya Ghuba yenye kambi za kijeshi za Marekani yamekuwa mara kwa mara yakishambuliwa na Iran tangu uchokozi wa Marekani na Israel uanze mwishoni mwa mwezi Februari.
Mashambulizi hayo ya leo yanakuja ikiwa ni siku moja tu baada ya Kuwait kusema mfanyakazi mmoja aliuawa baada ya mashambulizi ya Iran kupiga kwenye jengo la kampuni ya Kichina kaskazini mwa nchi hiyo.
Israel yaripuwa karibu na Beaufort
Kwenye upande mwengine wa vita hivi, Israel ililishambulia eneo lililo kwenye orodha ya Turathi za Ulimwengu ya UNESCO kusini mwa Lebanon siku ya Ijumaa.
Jeshi la Israel lilisema lilikuwa limeshambulia kwa mabomu ya kupasua miamba kuzunguka ngome mashuhuri ya Beaufort, likidai kuzilenga njia za chini kwa chini zinazotumiwa na kundi la Hizbullah linaloungwa mkono na Iran.
Shirika la habari la Lebanon lilithibitisha mashambulizi hayo, ambayo yalitajwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wake wa ulinzi, Israel Katz, kuwa ni ulipizaji kisasi baada ya kundi la Hizbullah kuvunja makubaliano ya usitishaji mapigano kati ya Tel Aviv na Beirut jana Jumatano, madai yanayokanushwa na Hizbullah, ambayo hata hivyo haiyatambui makubaliano hayo.
Spika wa Bunge la Lebanon, Nabih Berri, aliyaita mashambulizi hayo kuwa ni uvunjaji wa makusudi wa makubaliano hayo na ambao "hautanyamaziwa kimya."