Iraq: Majeshi yadhibiti majengo ya serikali
7 Machi 2017Eneo hilo lenye majengo mengi ya serikali ambayo ni pamoja na makao makuu ya baraza la jimbo, lipo katika mji jirani wa Dawasah ambako mapigano yamekuwa yakiendelea kwa siku mbili.
Majeshi yanayoungwa mkono na Marekani yalifanikiwa kulidhibiti daraja la al-Hurriya linalopita mto Tigris. Daraja la al-Hurriya ni la pili kurejeshwa na majeshi hayo, kati ya madaraja matano makubwa yanayounganisha kingo za Kushoto na Kulia za mto Tigris katika mji huo.
Mashambulizi haya yaliyodumu kwa zaidi ya wiki mbili sasa tangu kuanza kwa hatua mpya za kuwaondoa wanamgambo wa kundi linalojiita Dola la kiislamu, IS katika eneo la Magharibi mwa Mosul yamekuwa ni pigo kubwa kwa kundi hilo la itikadi kali ambalo lilikuwa likishikilia karibu theluthi ya Iraq.
Kikosi maalumu kwa kushirikiana na jeshi la polisi vimefanikiwa kurejesha makao makuu ya polisi ya jimbo majengo ya mahakama na majengo ya idara za maji, umeme na maji taka.
Majeshi ya Iraq yalitangaza ukombozi kamili wa eneo la Mashariki mwa Mosul mnamo mwezi Januari baada ya kuanzisha rasmi operesheni ya kuurejesha mji huo mwezi Oktoba mwaka jana.
Kituo binafsi cha televisheni chenye makao yake Lebanon Al-Mayadeen kimeonyesha picha za moja kwa moja kutoka Mosul, za moshi mzito mweusi ukitokea maeneo tofauti ya Mosul. Picha hizo pia zilionyesha kile kilichoelezwa kuwa ni milipuko iliyotokana na mashambulizi mawili ya kujitoa muhanga yaliyofanywa na wanamgambo wa IS dhidi ya vikosi vya usalama vya serikali.
Katika hatua nyingine, taarifa kutoka ofisi za waziri mkuu wa Iraq zimesema, Waziri mkuu Haider al-Abadi amewasili katika mji huo wa Mosul kukagua vikosi vinavyofanya operesheni hiyo inayolenga kuwafurusha wanamgambo wa kundi la IS katika mji huo. Al-Abadi ni amiri jeshi mkuu wa majeshi ya Iraq.
Aidha, taarifa kutoka duru za kijeshi zinasema, Brigedia Generali Matthew Islaer kutoka muungano wa majeshi ya jumuiya za kimataifa nchini Iraq amenukuliwa akisema vikosi vya serikali vinavyopigania eneo la Mashariki mwa Mosul havijajipanga vyema na baadhi ya wapiganaji wa nje wanaanza kuondoka kwenye mji huo.
Amesema, vikosi vya serikali hata hivyo vinakabiliwa na mashambulizi makali katika vita hivyo ingawa anaamini vitafanikiwa.
Mosul ni mji wa pili kwa ukubwa nchini iraq, na ni eneo la mwisho muhimu la mji ambalo bado linashikiliwa na wanamgambo wa IS nchini humo. Mosul ilianguka katika mikono ya IS katika majira ya joto mwaka 2014, pamoja na eneo kubwa la Kaskazini na Magharbi mwa Iraq.
Mwandishi: Lilian Mtono.
Mhariri: Yusuf Saumu