Mabadiliko ya hali ya hewa yasababisha dhoruba Iraq
16 Mei 2022Hii ni mara ya nane kwa dhoruba kutokea kwenye nchi hiyo tangu katikati ya mwezi wa Aprili, ambayo tayari imekumbwa na mmomonyoka wa udongo, ukame na mvua kidogo, inayohusishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Mara ya mwisho dhoruba iliokea mwanzoni mwa mwezi huu na kusababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi 5,000 walilazwa hospitalini kutokana na matatizo ya kupumua.
Kulingana na shirika la habari la AFP, siku ya Jumatatu dhoruba ya mchanga ilitokea mji mkuu wa Baghdad pamoja na mji wa Shiite wa Najaf upande wa kusini, na Sulaimaniyah, katika eneo la kaskazini mwa Wakurdi, na kuleta uharibifu wa paa za nyumba na magari.
Vituo vya afya vilisalia wazi nchi nzima
Aidha dhoruba hiyo imeleta uharibifu katika uwanja wa ndege wa Baghdad, na kusababisha mamlaka kufunga anga na kusimamisha safari za ndege, shirika la habari la serikali la INA limesema.Viwanja vya ndege vya Najaf na Sulaimaniyah pia vilifungwa kwa siku hiyo.
Mamlaka katika majimbo saba kati ya 18 ya Iraq, ikiwa ni pamoja na Baghdad, waliamuru kufunga ofisi zote za serikali.
Vituo vya afya vilibaki wazi nchini nzima, mamlaka imeonya kuwa, wazee na watu wanaougua magonjwa sugu ya kupumua na magonjwa ya moyo ndiyo waliopo hatarini zaidi.
Mashariki ya Kati daima imekuwa ikikumbwa na dhoruba hizo za mara kwa mara,katika miaka ya hivi karibuni. Hiyo imesababishwa na matumizi makubwa ya maji ya mito na mabwawa, malisho ya mifugo kupita kiasi na ukataji miti ovyo.
Onyo la dhoruba ya mchanga
Iraq ni nchi yaenye utajiri wa mafuta na inajulikana kama nchi yenye mito maarufu miwili, ambayo ni Tigris na Euphrates.
Lakini usambazaji wa maji umepungua kwa miaka mingi na ni miongoni mwa nchi tano duniani ambazo ziko hatarini zaidi kwa mabadiliko ya hali ya hewa na kuenea kwa jangwa.
Mnamo Aprili, afisa wa wizara ya mazingira Issa al Fayad alionya kwamba Iraq inaweza kukabiliwa na "siku 272 za dhoruba ya mchanga" kwa mwaka katika miongo miwili ijayo.
Ukame na joto kali imekausha mashamba nakupelekea watu kushindwa kuishi sehemu kubwa ya Iraq wakati wa kiangazi. Nchi hiyo imekuwa na rekodi ya kiwango cha joto 52 digrii Celsius katika miaka ya hivi karibuni.
Benki ya Dunia imeonya kuwa Iraq huenda ikapoteza asilimia 20 ya rasilimali za maji ifikapo 2050.