Iraq yalalamikia mashambulizi ya Uturuki
17 Desemba 2007Ndege za Kijeshi za Uturuki, jana asubuhi zilifanya mashambulizi makubwa katika makambi ya wanamgambo wa chama kilichopigwa marufuku nchini Uturuki cha Kurdistan Workers Party PKK.
Chama hicho cha PKK kinapigana kutaka kujitenga kwa eneo la kusini mashariki mwa Uturuki toka mwaka 1984 na serikali ya uturuki inakihesabu kuwa ni kikundi cha kigaidi.
Viongozi wa Iraq wamesema kuwa Uturuki imefanya mashambulizi hayo bila ya kuwasiliana nao.Mashambulizi hayo ya jana ni makubwa kufanywa na jeshi la anga la Uturuki katika miaka ya hivi karibuni.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq Hoshyar Zebari amesema kuwa serikali yake ilitegemea Uturuki ingewasiliana nao kwanza kabla ya kufanya mashambulizi hayo.
Matokeo yake amesema kuwa waliyoathirika na mashambulizi hayo ni raia wa Iraq na siyo wapiganaji wa PKK waliyoko nchini Irak.
Lakini Uturuki kwa upande wake imesisitiza kuwa malengo ya mashambulizi hayo yalifanikiwa.
Pamoja na serikali ya Uturuki kutotoa taarifa rasmi juu ya hasara za mashambulizi hayo, lakini shirika la habari lenye kuegemea upande wa PKK liitwalo FIRAT linasema kuwa watu wameuawa wakiwemo waasi watano na raia wawili.
Maafisa wa Iraq wamesema kuwa mashambulizi hayo ya jana asubuhi yamesababisha kifo cha mwanamke mmoja na wengine watano kujeruhiwa ikiwa ni pamoja na kuharibiwa vibaya kwa madaraja na shule kwenye eneo hilo la Qandil.
Mzee mmoja Hassan Ibrahim mkulima katika kijiji cha Qalatuga kilichoko mpakani mwa Iraq na Uturuki amesema kuwa walikuwa wamelala wakati ndege za Uturuki ziliangusha mabomu kijijini kwao.
Mzee huyo kwa hasira anasema kuwa mwanzo waliitaabishwa na Saddam Hussein kwa kuvunjiwa majumba yao na sasa ni waturuki.
Mjini Ankara vyombo vya habari habari vya Uturuki vimeripoti leo kuwa mkuu wa tawia la kijeshi la PKK Murat Karayilah ndiyo aliyekuwa lengo kuu la mashambulizi hayo.
Magazeti matatu ya kila siku nchini humu, Sabah,Aksam na Yeni Safak yamearifu kuwa Karayilah ndiyo alikuwa mlengwa wa mashambulizi hayo, lakini alikimbia baada ya kubaini kuwepo kwa mashambulizi hayo kwa kutumia simu yake ya setelite.
Karayilah ambaye alikuwa mpambe wa karibu wa kiongozi wa chama hicho cha PKK aliyekifungoni, Abdullah Ocalen anaongoza kundi la wanamgambo waliyoko kusini mwa Iraq.
Kundi hilo la PKK ambalo Marekani na Ulaya zimeliweka katika orodha ya makundi la kigaidi, linakadiriwa kuwa wapiganaji takriban 3,500 ndani ya Iraq.
Toka kundi hilo la PKK lilipoanzisha harakati zake za kutaka kujitenga kwa eneo la kusini mashariki mwa Uturuki mwaka 1984, zaidi ya watu elfu 37 wamekwishauawa.