1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iraq yalikomboa Bwawa la mosul

18 Agosti 2014

Wapiganaji wa Kikurdi nchini Iraq wamefanikiwa kulikomboa tena bwawa kubwa la Mosul kutoka kwa wanamgambo wa kundi la dola la kiislamu la Iraq.

Wapiganaji wa Kikurdi
Wapiganaji wa KikurdiPicha: AHMAD AL-RUBAYE/AFP/Getty Images

Bwawa hilo limekombolewa huku Marekani ikiendelea na mashambulizi ya anga kwa siku ya pili katika eneo hilo kwa lengo la kuitwaa miji inayoshikiliwa na wanamgambo hao wanaolidhibiti eneo kubwa la kaskazini mwa Iraq.

Televisheni ya taifa ya Iraq, imemnukuu msemaji wa jeshi, Luteni Jenerali Qasim Atta, akisema kwamba vikosi vya Wakurdi vimefanikiwa kulitwaa bwawa hilo kwa msaada wa mashambulizi ya anga yaliyofanywa kwa ushirikiano wa vikosi vya kupambana na ugaidi.

Hata hivyo, hakutoa ufafanuzi zaidi. Katika wiki za hivi karibuni, kundi la waasi linalojiita Dola la Kiislamu liliitwaa miji kadhaa na maeneo ya kuchimba mafuta pamoja na bwawa kubwa la Mosul.

Afisa wa Kikurdi, amesema kwa sasa wanalidhibiti tena bwawa hilo ingawa sehemu kubwa ya maeneo inayolizunguka, inadhibitiwa na waasi. Marekani imesema imefanya mashambulizi 14 ya anga jana Jumapili, dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu karibu na bwawa hilo.

Kamanda mkuu wa Marekani amesema mashambulizi ya hivi karibuni, yamefanyika baada ya mashambulizi mengine tisa ya angani yaliyofanywa siku ya Jumamosi karibu na bwawa la Mosul na mji mkuu wa jimbo la Kurdistan, Arbil.

Frank Walter-Steinmeier akiwa na Hussein Al-ShahristanPicha: Reuters

Obama alilitaarifu Bunge

Ikulu ya Marekani ilisema jana kwamba Rais Barack Obama, aliliarifu Bunge kufuatia hatua yake ya kuidhinisha mashambulizi ya anga yatakayofanywa na ndege zake za kivita kwa ajili ya kulidhibiti tena bwawa hilo muhimu linalosambaza nguvu za umeme katika eneo hilo zima. Watu walioshuhudia wamesema kuwa vikosi vya Kikurdi vimeitwaa tena miji yenye Wakristo ya Batmaiya na Telasqaf, iliyoko umbali wa kilomita 30 kutoka Mosul.

Kukombolewa tena kwa bwawa hilo lililotekwa wiki iliyopita, kunaashiria ushindi mkubwa wa kwanza dhidi ya wapiganaji wa jihadi wa kundi hilo tangu walipoanzisha mashambulizi yao kaskazini mwa Iraq mwezi Juni mwaka huu.

Wakurdi wanaoishi kwenye eneo hilo lililojitangazia utawala wake katika eneo la kaskazini, wanataka uhuru wao kutoka serikali kuu ya Iraq. Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank Walter-Steinmeier, ameonya dhidi ya hatua ya kuanzishwa kwa taifa huru la Wakurdi, akisema kwamba itahatarisha zaidi hali ya kuwepo utulivu kwenye eneo hilo.

Watu wa jamii ya Yazidi wakiyakimbia mapiganoPicha: Reuters

Steinmeier aliyekutana na Waziri Mkuu mpya wa Iraq, Haider al-Abadi, siku ya Jumamosi alisema nchi yake itapeleka msaada zaidi wa kibinaadamu kwa watu wa jamii ya Yazidi wanaokabiliwa na kitisho kutoka kundi la Dola la Kiislamu. Naibu Waziri Mkuu wa Iraq, Hussein Al-Shahristan amewataka watu wa jamii ya wachache kutoyakimbia makaazi yao na ameahidi kulindwa na kujengwa upya kwa miji yao.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron alisema jana kuwa Uingereza inapaswa kutumia uwezo wake wa kijeshi kukabiliana na wapiganaji wa Dola la Kiislamu, ili kuwazuia wasianzishe hali ya kuwepo taifa la kigaidi katika mwambao wa Bahari ya Mediterania.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,APE
Mhariri: Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW