Iraq yaomba msaada kwa Marekani
19 Juni 2014Rais wa Marekani hapo jana aliwahutubia viongozi wa bunge la Congress juu ya hatua za kukabiliana na wanamgambo wa kundi la kigaidi, la dola la kiislamu la Iraq na eneo la Sham ISIL, lililoanzisha mashambulizi nchini Iraq takriban wiki moja iliopita.
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iraq Hoshyar Zebari amethibitisha kuwa nchi yake imeiomba rasmi Marekani kutekeleza shambulizi la angani katika maeneo yanayoshikiliwa na wanamgambo wa ISIL.
Amesema dunia nzima inapaswa kuisaidia Iraq kupambana na kundi hilo. "Tunakubali kuwa Iraq iko hatarini na inahitaji uungwaji mkono wa mataifa ya kiarabu na dunia nzima kusimamisha uasi huu.
Hatari ya kugawika kwa taifa hili ipo na hili likifanyika hali itakuwa mbaya zaidi kuliko Syria," Alisema Waziri Zebari.
Hata hivyo Obama bado hajaondoa uwezekano wa kutekeleza shambulizi hilo la angani huku maafisa wa usalama wa Marekani wakisema hatua hiyo haitakuwa ya hivi karibuni kwa sababu mashirika yake ya kijasusi yameshindwa kutambua maeneo halisi ya kulengwa wanamgambo hao.
Badala yake Marekani imeisukuma Iraq kutoa mwelekeo na muungano wa wazi kwa watu wake juu ya namna ya kupambana na wanamgambo.
Makamu wa rais wa Marekani Joe Baiden amependekeza kuwepo na mazungumzo na viongozi wa madhehebu ya Shia, Sunni na Kurdi ili kutatua mgogoro unaoendelea kupamba moto nchini humo.
Mashambulizi bado yanaendelea katika eneo la Baiji
Naye Waziri Mkuu wa Uturuki Tayyip Erdogan amesema iwapo Marekani itatekeleza mashambulizi hayo ya angani huenda hatua hiyo ikasababisha mauaji zaidi ya raia wa Iraq na kwamba kwa sasa Marekani haioneni kwamba hiyo ndio suluhu inayofaa.
Kwa upande wake taifa la falme za kiarabu ambaye ni mshirika mkuu na mfanyabiashara mkubwa wa Iraq limemuondoa balozi wake nchini Iraq kwa mazungumzo. Kulingana na wizara ya mambo ya nchi za nje ya UAE taifa hilo lina wasiwasi juu ya sera ya kidini ya Iraq.
Huku hayo yakiarifiwa mapigano yamezidi kuripotiwa nchini Iraq. Polisi pamoja na wataalamu wa afya wameripoti kuwa gari moja limeripuka ndani ya eneo la kuegesha magari mjini Baghdad katika eneo linalokaliwa na washia. Watu watatu wameuwawa huku wengine saba wakijeruhiwa katika shambulizi hilo.
Aidha zaidi ya wafanyakazi 250 waliokuwa wamenasa katika kinu kikubwa cha mafuta nchini Iraq cha Baiji wameachiwa baada ya makabiliano ya muda mfupi kati ya wanajeshi wa Iraq na wanamgambo wa madhehebu ya sunni. Hii ni Kulingana na moja ya wafanyakazi walioachiwa.
Kinu hicho cha mafuta cha Baiji kina wafanyakazi 15,800 pamoja na wataalamu 100 wa kigeni, ambapo wengi wao waliondoka siku ya jumaane baada ya serikali kukifunga kwa hofu ya mashambulizi yaliofanyika mapema siku ya Jumatano.
Mwandishi: Amina Abubakar/AP/Reuters
Mwandishi: Josephat Charo