1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iraq yataka wanajeshi wa Marekani waondoke nchini humo 

Zainab Aziz Mhariri:Gakuba, Daniel
6 Januari 2020

Bunge la Iraq limepiga kura ya kuwafukuza wanajeshi wa Marekani kutoka nchini humo.Hatua ya bunge la Iraq itawahusu wanajeshi wengine wa kimataifa kuondoka nchini humo ikiwa ni pamoja na wanajeshi wa Ujerumani.

Irak Bagdad | Parlamentssitzung
Picha: Reuters/Iraqi parliament media office

Huku mvutano baina ya Marekani na Iran ukizidi kupamba moto bunge la nchini Iraq hapo siku ya Jumapili lilipiga kura ya kuwaondoa wanajeshi wa Marekani kutoka Iraq. Katika kikao kisicho cha kawaida wabunge waliridhia azimio la kuitaka serikali kufuta makubaliano na Marekani kuhusu kuwepo wanajeshi wake wapatao 5,200 nchini Iraq.

Azimio hilo lililopitishwa siku ya Jumapili linalenga kuyafuta makubaliano ya mwaka 2014 ambayo yaliiruhusu Marekani kuwapeleka wanajeshi wake nchini Iraq kusaidia katika mapambano dhidi ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS. Azimio la serikali ya Iraq limebaini kuwa sasa nchi hiyo imeamua kulifuta rasmi ombi lake la kutaka msaada wa vikosi vya kimataifa katika mapambano dhidi ya IS kwa sababu zoezi hilo limemalizika kwa mafanikio.

Kwa upande wake Rais wa Marekani Donald Trump amesema baada ya bunge la Iraq kupiga kura siku ya Jumapili, Marekani haitaondoka kutoka nchini humo bila ya kulipwa kwa uwekezaji wake wa kijeshi nchini humo kwa miaka kadhaa. Trump amesema ikiwa wanajeshi wa Marekani wataondoka, hatosita kuiwekea Iraq vikwazo vya kiuchumi.

Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Imago Images/UPI Photo/G. Rothstein

Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas amesema jamii ya kimataifa imefanya mengi kuleta utulivu na kuijenga tena Iraq na kwamba juhudi zote hizo zinakabiliwa na hatari ya kupotea ikiwa hali itaendelea kama ilivyo sasa. Maas amesema haitasaidia kuitishia Iraqi baada ya bunge lake kupiga kura ya kuwafukuza wanajeshi wa Marekani kutoka nchini humo.

Wakati huo huo China imeilaumu Marekani kwa kuchochea mvutano unaozidi kuwa mkubwa katika eneo la Mashariki ya Kati kutokana na matumizi ya nguvu katika mfarakano baina yake na Iran. China imesema tabia hatari ya kijeshi ya Marekani katika siku za hivi karibuni ni kinyume cha kanuni za msingi za uhusiano wa kimataifa.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Geng Shuang amesema matumizi ya nguvu hayana uungwaji mkono wa umma na wala hayatoi suluhisho la kudumu katika mvutano baina ya Marekani na Iran.

Spika wa Bunge la Marekani Nancy Pelosi amesema bunge litawasilisha na kulipigia kura azimio kuhusu nguvu za Rais kuamuru hatua za kijeshi dhidi ya Iran wiki hii ili kumuwekea kikomo Rais Donald Trump.

Azimio hilo bila shaka litapitishwa katika bunge linalodhibitiwa na chama Democratic lakini hakuna matarajio ya kuidhinishwa katika baraza la Seneti linalodhibitiwa na chama cha Republican ambapo wajumbe wengi wamesema wanaiunga mkono hatua ya Rais Trump juu ya Iran. Mabalozi wa nchi wanachama wa NATO watakutana leo Jumatatu mjini Brussels kujadili mvutano wa Mashariki ya Kati unaongezeka baada ya vikosi vya Marekani kumuua jenerali Qasem Soleimani wa Iran.

Vyanzo:RTRE/AP/AFP/https://p.dw.com/p/3Vji4

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW