1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iraq: Zogo huenda likazuka kati ya Uturuki na waasi wa PKK

Mwakideu, Alex25 Februari 2008

Mshauri wa maswala ya usalama nchini Iraq Mowaffaq al-Rubaie amesema uvamizi unaoendelezwa na Uturuki huenda ukaleta masaibu makubwa

Waandamanaji wapinga mashambulizi ya waasi wa KikurdiPicha: AP

Uvamizi unaoendelezwa na majeshi ya Uturuki kaskazini mwa Iraq huenda ukazua mgogoro kati ya majeshi hayo na wapiganaji wa jimbo hilo la Kurdistan linalojisimamia. Hayo ni kwa mujibu wa mshauri wa usalama nchini Iraq.


Mshauri huyo Mowaffaq al-Rubaie ameongezea kwamba uvamizi kama huo utaleta masaibu makubwa katika eneo ambalo limekuwa na utulivu wa likilinganishwa na maeneo mengine nchini humo.


Uvamizi wa Uturuki ulianza alhamisi katika maeneo ya mashinani mwa jimbo linalojitawala Kurdistan ukilenga kuwamaliza waasi wa kikurdi wa PKK.


Uturuki inashutumu waasi hao kwa kutumia maeneo ya kaskazini mwa Iraq kama makao ya kupanga mashambulizi dhidi yake.


Rubaie amesema wanajeshi wa Uturuki wanapoendelea kukaa nchini Iraq basi huenda kukazuka zogo kati yao na wapiganaji wa Peshmerga.


Amesema itakuwa muhimu iwapo zogo hilo litazuiliwa kabla halijazuka kwani litakapozuka litaleta hasara kubwa.


Mlinda usalama mmoja wa kikurdi ameelezea makabiliano aliyoshuhudia kati ya vikosi vya Uturuki na waasi wa Kurdistan Workers Party (PKK) usiku wa jana katika maeneo ya Amidiya kilomita 10 kusini mwa mpaka wa nchi hizo mbili.


Vyombo vya habari nchini Uturuki vimeripoti leo kwamba majeshi ya nchi hiyo yanaelekea katika makao makuu ya waasi wa PKK katika milima ya Qandil karibu na mpaka wa Iraq na Iran.


Gazeti la Hurriyet limeripoti kwamba kambi za waasi wa PKK katika majimbo ya Zap na Bonde la Cemco yaliharibiwa mwishoni mwa wiki na kwamba majeshi ya Uturuki yakiwa na ndege za kivita aina ya F-16 yanalenga makao makuu ya waasi hao huko Qandil


Msemaji wa Uturuki Cemil Cicek ametetea uvamizi huo akisema kwamba Uturuki inakubaliwa na sheria za kimataifa kujikinga dhidi ya waasi wa PKK wanaotumia Iraq kama makao ya kushambulia raia na majeshi wa nchi yake.


Cicek amesema Uturuki ililazimika kuvamia waasi hao baada ya kuomba msaada wa majeshi ya Marekani walioko nchini Iraq na hata majeshi ya Iraq bila kufaulu.


Amesema watu wa Iraq ni marafiki wa Uturuki na kwamba nia ya uvamizi huo ni kukabiliana na waasi hao wa PKK pekee.


Kwa upande mwingine waziri wa mambo ya nchi za nje nchini Iraq Hoshiar Zedari ameelezea hofu yake kwamba uvamizi huo ukiendelea huenda ukazua hasara kubwa kwa watu wa Iraq Kaskazini.


Hata hivyo msemajiw a wa serikali ya Uturuki amesema vikosi vya nchi hiyo vitarejea nyumbani punde tu vitakapofaulu kuharibu uwezo wa waasi wa PKK wa kuvuka mpaka na kuingia nchini humo kwa nia ya kushambulia. Hata hivyo hakuweza kusema uvamizi huo utamalizika lini.


Kulingana na taarifa iliyotolewa na Uturuki mwishoni mwa wiki watu 127 wameuwawa tangu nchi hiyo ianze uvamizi wake alhamisi wiki jana. Kati ya hao ni waasi 112 wa PKK na wanajeshi 15 wa Uturuki. Hata hivyo waasi wa PKK wamepinga taarifa hizo.


Marekani na Umoja wa Ulaya zinaitambua PKK kama shirika la kigaidi.


Rais wa Uturuki Abdullah Gul amelazimika kukatiza ziara yake barani Afrika kutokana na uvamizi huo unaoendelea.


Gul alitarajiwa kusafiri kesho kuelekea nchini Tanzania na kisha Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo pamoja na Jamhuri ya Congo.


Hii leo rais huyo amepiga ziara ya ghafla kwa makao makuu ya jeshi la nchi hiyo jijini Ankara na kupewa arifa kuhusu uvamizi huo.


Maafisa wa Marekani wamesema Uturuki imehakikisha kwamba itafanya kila iwezalo isisababishe maafa yoyote kwa raia wa kawaida walioko kaskazini mwa Iraq.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW