1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iraqi yaurejesha mji wa kale wa Nimrud

14 Novemba 2016

Majeshi ya Iraqi jana jumapili(13.11.2016) yamefanikiwa kuurejesha mji wa kale wa  kihistoria ulioharibiwa na mashambulizi ya  kundi la Dola la Kiislamu, IS.

Irak Zerstörung antike Stadt Nimrud durch Islamischer Staat
Picha: picture-alliance/dpa/militant webside

Mnamo mwaka 2014, kundi la Dola la kiislamu liliharibu baadhi ya vitu vya kale ambavyo shirika la Umoja wa mataifa linaloshughulikia vitu vya kale, UNESCO, lilitaja mashambulizi hayo kama uhalifu wa kivita.

Majeshi ya Iraqi Jana yalifanikiwa kuurejesha mji wa kihistoria wa Nimrud, hatua inayoonyesha kusonga mbele kwa majeshi hayo katika kampeni yake ya kuwafurusha wapiganaji wa kundi la Dola la kiislamu, IS, amesema kiongozi wa kamandi ya muungano kwenye operesheni hiyo ya kuukomboa mji wa Mosul.

Kiongozi wa kampeni hiyo kutoka serikalini, Abdul Amir Rasheed, amesema vikosi vilivyokuwa na silaha vimefanikiwa kuuchukua mji huo wa Nimrud na kupandisha bendera za Iraqi kwenye majengo yake. Hata hivyo baadhi ya maafisa wa jeshi wameviambia vyombo vya habari kwamba bado vikosi vinaendelea kuwasaka wapiganaji hao na kulipua baadhi ya mabomu yaliyotegwa kwenye maeneo mbalimbali.

Nimrud ulikuwa ni miongoni mwa maeneo muhimu ya kihistoria katika Mashariki ya kati ya zamani, uliotambuliwa katika karne ya 13. Ulitambulikana kama mji mkuu wa kihistoria kile kilichokuwa kikijulikana kama ufalme wa Assyrian  ambapo watawala walijenga majengo makubwa yaliyokuwa na michoro ya kale kwa zaidi ya miaka 150.

Askari wa usalama akilinda sehemu ya majengo ya historia yaliyoko NimrudPicha: picture-alliance/dpa/S. Baldwin

Mashambulizi ya kujitoa muhanga yaendelea kufanywa na IS.

Katika hatua nyingine, mashambulizi yasiyo ya kawaida ya kujitoa muhanga yaliyofanywa leo hii kwenye mji wa Oasis ilioko Kusini mwa mwa Baghdad yamesababisha mauaji ya raia wanane na wengine sita kujeruhiwa. Maafisa wa Iraqi wamesema, mashambulizi hayo yalihusisha washambualiaji sita waliojitoa muhanga, ambao miongoni mwao waliuwawa na vikosi vya usalama kabla ya kujilipua.  

Mjumbe wa baraza la jimbo la Karbala, Masum al- Tamimi, amesema washambuliaji sita walikuwa na silaha nyepesi, pamoja mabomu na kujaribu kujipenyeza kwenye eneo la Ain al-Tamer maepam leo hii. Hata hivyo walikabiliwa na vikosi vya usalama kabla ya kutoroka amesema Tamimi. Taarifa za madaktari zinasema, watu wanane waliuwawa. 

Wizara ya mambo ya ndani imetoa taarifa kuhusiana na shambulizi hilo inayosema washambuliaji watano waliuwawa na vikosi vya usalama, wakati mshambuliaji wa sita alifanikiwa kujilipua akiwa ndani ya nyumba. Hata hivyo hakuna taarifa yoyote ya mapema iliyotolewa kuhusiana na muhusika wa shambulizi hilo, ingawa inaelezwa kuwa kundi la Dola la Kiislamu limekuwa likihusika na mashambulizi kama hayo nchini Iraqi.

Kundi hilo la wapiganaji lilichukua eneo kubwa Kasikazini na Magharibi mwa Baghdad mnamo mwaka 2014, ingawa vikosi vya usalama vinavyosaidiwa na Marekani kwa kufanya mashambulizi ya angani kwa pamoja wamefanikiwa kurejesha sehemu kubwa ya eneo lililoshikiliwa na kundi hilo la wapiganaji miaka miwili iliyopita.
 
Mwandishi: Lilian Mtono/AFPE.
Mhariri: SaumuYusuf

http://www.dw.com/en/iraq-claims-victory-over-islamic-state-in-nimrud/a-36377501