IRGC yatishia kulenga maeneo mapya ya Marekani
21 Septemba 2026
Katika taarifa yake, msemaji wa IRGC amesema kutakuwa na mabadiliko makubwa katika mfumo wao wa ulinzi na mashambulizi ya kisasi ikiwa Marekani itafanya shambulio jipya dhidi ya Iran.
Jeshi hilo pia limesema kuwa litaleta silaha mpya zenye uwezo mpya katika uwanja wa vita, na kuishangaza dunia. Taarifa hiyo imeongeza kuwa shabaha zao hazitakuwa kama za awali na kwamba wana maeneo mapya ambayo hayajawahi kushambuliwa.
IRGC imesema iko tayari kwa "vita vya muda mrefu."
Siku ya Jumamosi, televisheni ya taifa iliripoti kuwa kamandi kuu ya jeshi la Iran ilisema Marekani ilikuwa inapanga mashambulizi mapya dhidi ya Tehran, lakini haikutoa maelezo zaidi kuhusu madai hayo.
Wahouthi wasema hawalengi meli za Marekani katika Bahari ya Shamu
Mohamed al-Bukhaiti, mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wahouthi, amesema kuwa Washington iliwasiliana na jeshi lao baada ya kusonga mbele kwa haraka katika pwani ya magharibi ya Yemen hadi kwenye Mlango Bahari wa Bab el-Mandeb mapema mwezi huu.
Katika mahojiano kwa njia ya video na shirika la habari la AP akiwa mjini Sanaa, mji mkuu wa Yemen, unaodhibitiwa na kikosi hicho cha waasi, al-Bukhaiti alithibitisha kwamba hawailengi Marekani, wala taifa jingine lolote, katika mlango huo wa bahari, isipokuwa adui wa pekee waliomtaja kuwa Saudi Arabia na kusema hali hiyo bado haijabadilika.
Wakati huo huo, mapigano ya hivi karibuni kati ya kundi hilo la Wahouthi na vikosi vya serikali yamesababisha zaidi ya watu 125,000 kuyahama makazi yao ndani ya Yemen katika kipindi cha wiki chache tu. Haya yamesemwa jana na Armen Yedgaryan, afisa wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) nchini Yemen.
"Kwa hivyo ni idadi kubwa sana tangu mwanzo wa ongezeko hili la hivi karibuni la mapigano. Wengi wa waliolazimika kuyahama makazi yao ni wanawake, watoto na wazee, idadi kubwa ya watu walio katika mazingira magumu sana ambao wanahitaji huduma za matibabu, malazi, chakula, maji na ulinzi. Walilazimika kukimbia ndani ya muda mfupi, wakiwa na mali kidogo au bila chochote," amesema Yedgaryan.
Raia wa Israel auawa kaskazini mwa Ramallah
Raia mmoja wa Israel ameuawa karibu na makazi ya Neve Tzuf, kaskazini mwa Ramallah, saa chache kabla ya kuanza kwa Yom Kippur, siku takatifu zaidi katika kalenda ya Wayahudi.
Jeshi la Israel limesema mshukiwa wa shambulio hilo alifyatua risasi akiwa ndani ya gari na kisha akatoroka kwa miguu. Baada ya operesheni ya kumsaka iliyofanywa na vikosi vya usalama, jeshi lilisema mtu huyo, ambaye alijeruhiwa alipokuwa akikimbia, alikamatwa katika hospitali ambako alikuwa ameenda kupata matibabu.
Katika taarifa yake, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ameyataja mashambulizi hayo kuwa "ya kuchukiza" na kuliagiza jeshi kuongeza operesheni zake katika Ukingo huo wa Magharibi.