IS waondoka ngome ya mwisho Damascus
20 Mei 2018Taarifa ya shirika hilo lenye makao yake London, Uingereza, iliyotolewa Jumapili (20 Mei) ilisema kuwa idadi rasmi ya wapiganaji waliondoka haikujulikana, lakini wao na familia zao walichukuliwa kwa mabasi kuondoka kwenye eneo la kusini mwa Damascus, wakielekea jimbo la mashariki la Deir al-Zour.
Kuondoka kwa wapiganaji kunakuja baada mapigano makali ya mwezi mzima yaliyoongozwa na vikosi vinavyomtii Rais Bashar al-Assad yaliyodhamiria kuliteka eneo hilo, likiwa la mwisho kabisa nje ya mji mkuu huu.
Eneo hilo, ambalo ni sehemu ya makubaliano yanayojumuisha kambi ya wakimbizi ya Yarmouk, liliripotiwa kuwa shwari tangu siku ya Jumamosi, kwa mujibu wa shirika hilo la haki za binaadamu.
Hata hivyo, shirika rasmi la habari la Syria, SANA, lilikanusha ripoti za kuondolewa kwa wapiganaji kutoka eneo hilo. Shirika hilo lilisema kwamba jeshi lilikuwa likisonga mbele na operesheni yake dhidi ya "magaidi" kusini mwa Damascus na kwamba lilikuwa limewarejesha nyuma hadi kwenye eneo dogo kabisa.
IS imepoteza takribani ngome zote
Mnamo mwezi uliopita (Aprili 2018), vikosi vya serikali vilitwaa tena udhibiti wa kitongoji cha Ghouta Mashariki, ambacho kiliwahi kuwa ngome kuu ya upinzani karibu na mji mkuu, Damascus.
Kukamatwa kwa Ghouta Mashariki kulichukuliwa kama ushindi mkubwa kabisa kwa Assad tangu Disemba 2016, wakati wanajeshi wake walipotwaa udhibiti wa mji wa kaskazini wa Aleppo, kufuatia mashambulizi makali yaliyosaidiwa na Urusi.
Bado Damascus inasalia kuwa ngome muhimu kwa Assad, ambaye katika miezi ya hivi karibuni, vikosi vyake vinavyosaidiwa na mashambulizi ya angani ya Urusi, vimepata mafanikio makubwa dhidi ya waasi na wanamgambo katika maeneo mbalimbali ya taifa hilo lililosambaratishwa kwa vita.
Kwa upande mwengine, wapiganaji wa Kikurdi na Kiarabu nao waliripotiwa kusonga mbele dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu mashariki mwa Syria, kwa msaada mkubwa wa mashambulizi ya angani kutoka kwa majeshi ya Marekani na Ufaransa.
Mapema mwezi huu, wapiganaji wa kikosi cha Syrian Democratic Forces (SDF) walifanya mashambulizi kwa msaada wa Marekani dhidi ya wanamgambo wa Dola la Kiislamu karibu na mpaka wa Iraq, ambako wanamgambo hao wakivikalia vijii vitatu vikubwa - Hajjin, Sousa na Al Shaafa.
Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AFP/AP
Mhariri: Jacob Safari