1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israe: Nusu ya wanamgambo wa Hamas wameuwawa

7 Juni 2024

Marekani na Israel zinadai takriban nusu ya wapiganaji wa kundi la wanamgambo la Hamas wameuawa katika miezi minane ya vita na sasa kundi hilo linafanya mashambulizi ya kuvizia dhidi ya vikosi vya Israel.

Marekani Israel | Joe Biden na Benjamin Netanjahu
Rais wa Marekani Joe Biden akiwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.Picha: Avi Ohayon/Israel Gpo/Zumapress/imago images

Maafisa wa Marekani wanadai kuwa idadi ya wapiganaji wa kundi hilo la wanamgambo imepungua hadi kufikia kati ya 9,000 na 12,000 kutoka makadirio ya wapiganaji kati ya 20,000 na 25,000 kabla ya vita kuanza. 

Kwa upande wake, Israel inadai kuwa imepoteza karibu wanajeshi 300 katika vita hivyo vya Gaza.

Wakaazi kadhaa wa Gaza, akiwemo Wissam Ibrahim, wanasema wao pia wameshuhudia mabadiliko ya kimbinu.

Ibrahim ameliambia shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu kwamba katika miezi ya mwanzo, wapiganaji wa Hamas wangeweza kuzuia na kuwashambulia wanajeshi wa Israeli mara tu walipoingia kwenye himaya zao, lakini sasa kuna mabadiliko ya wazi katika jinsi wanavyofanya operesheni zao ambapo kwanza wanawasubiri kufika katika maeneo hayo kisha kuanza uvamizi na mashambulizi.

Soma pia:Israel yatahadharishwa dhidi ya kuanza kushambulia Rafah

Maafisa hao wa Marekani wamesema mbinu hizo zinaweza kuendeleza uasi wa Hamas kwa miezi kadhaa ijayo, wakisaidiwa na silaha zilizoingizwa kimagendo Gaza kupitia njia za chini ya ardhi na nyingine zilizotengenezwa upya kutoka kwa mabomu ya Israel ambayo hayakuripuka ama yaliyokamatwa na wanamgambo hao.

Kuongezeka kwa muda wa uasi wa Hamas, pia kumesisitizwa na mshauri  wa usalama wa kitaifa wa Netanyahu ambaye wiki iliyopita alisema kuwa vita vinaweza kudumu hadi mwisho wa mwaka 2024.

Msemaji wa kundi la Hamas, hakujibu ombi la kutoa tamko kuhusu mbinu hizo za kivita.

Propaganda katikati ya vita

Baerbock ziarani Israel tena kusaka suluhisho la mgogoro

02:41

This browser does not support the video element.

Katika harakati nyingine za propaganda, baadhi ya wapiganaji wa kundi hilo la Hamas, wanarekodi video za uvamizi wao dhidi ya vikosi vya Israel, kabla ya kuhariri na kuzichapisha kwenye mtandao wa Telegram na mingine ya kijamii.

Peter Lerner, msemaji wa Jeshi la Israel, ameiambia Reuters kwamba bado wana kibarua kigumu katika kulisambaratisha kundi la Hamas licha ya kusisitiza pia kuwa kundi hilo limepoteza takribani nusu ya wapiganaji wake.

Lerner amesema jeshi la nchi yake limeanza kuzowea mabadiliko ya kundi hilo la Hamas katika uwanja wa vita na kukiri kuwa Israel haijaweza kukabiliana na wapiganaji wote ama kuharibu kila handaki la Hamas.

Soma pia:Jeshi la Israel limesema vikosi vyake sasa vinaendesha shughuli zake mjini Gaza.

Lerner ameongeza kuwa hakuna lengo la kuwaangamiza wapiganaji wote na kwamba hilo sio lengo linalowezekana.

Netanyahu na serikali yake wanashinikizwa na Marekani kukubaliana na mpango wa kusitisha mapigano ili kumaliza vita, vilivyoanza Oktoba 7 wakati wapiganaji wa Hamas walipovamia kusini mwa Israel, na kusababisha vifo vya takribani watu 1,200 na kuwachukuwa mateka zaidi ya watu 250, kwa mujibu wa Israel.

Athari za vita vinavyoendelea

Mashambulizi ya angani na ardhini ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza yameliwacha eneo hilo kuwa na magofu na kuua zaidi ya watu 36,000, kwa mujibu wa wizara ya afya ya huko.

Mkaazi wa Gaza akitembelea masalia ya jengo lbaada ya kushambuliwa makaazi katika eneo hilo kushambuliwa na jeshi la Israel.Picha: Enas Rami/AP/picture alliance

Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya watu milioni moja wanakabiliwa na viwango vya juu vya njaa.

Marekani na Israel zinakisia kuwa kuna wapiganaji takribani 7,000 hadi 8,000 wa Hamas katika mji wa Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza, hii ikiwa ngome muhimu ya mwisho ya kundi hilo.

Soma pia:Antony Blinken asema hali ya Gaza inazidi kuwa mbaya

Viongozi wakuu wa Hamas Yahya Sinwar, kaka yake Mohammed na naibu wa Sinwar, Mohammed Deif bado wako hai na wanaaminika wamejificha kwenye mahandaki wakiwa pamoja na mateka wa Israel.

Afisa mmoja wa utawala wa Marekani, amesema kundi hilo la Hamas limeonyesha uwezo wa kujiondoa haraka baada ya mashambulizi, kujificha, kujipanga upya, na kuibuka tena katika maeneo ambayo Israel iliamini imeshayasafisha kabisa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW