1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel haitaondoka Lebanon, hadi Kikosi cha kimataifa kitakapowasili

Munira Muhammad16 Agosti 2006

Baraza la mawaziri la Lebanon linakutana leo jioni kutoa rasmi amri ya wanajeshi wake 15,000 kuelekea kusini mwa nchi hiyo.

Mwanajeshi wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon.
Mwanajeshi wa Umoja wa Mataifa nchini Lebanon.Picha: AP

Na huku Umoja wa Mataifa ukiharakisha mpango wa kutuma kikosi chake cha wanajeshi 3,500, Israel imesema haitaondoa wanajeshi wake nchini Lebanon hadi pale kikosi cha kimataifa kitakapowasili.

Huku Lebanon ikipumua kwa mashambulizi yaliochukua mwezi mzima, Umoja wa Mataifa sasa unajizatiti kutekeleza kwa haraka jukumu lake la kupeleka kikosi cha kimataifa cha wanajeshi wapatao 3,500 wa kuweka amani nchini Lebanon.

Licha ya ahadi za mataifa mbali mbali kuwa watatoa wanajeshi, hadi kufikia sasa hakuna nchi yeyote iliyotoa wanajeshi….kisa na maana jukumu la jeshi hilo bado halijafafanuliwa vyakutosha.

Mkuu wa jeshi la Umoja wa Mataifa, UNIFIL. Major generali Alain Pellegrini baada ya mkutano na maafisa wa jeshi wa Israel na Lebanon amesema huenda kikosi cha kimataifa kikachukua muda kuwasili nchiniu Lebanon.

Israel nayo imesema haitaondoa baadhi ya wanajeshi wake nchini Lebanon hadi pale kikosi cha kimataifa kitakapowasili.

Mjini Beirut baraza la mawaziri la Lebanon, linakutana leo jioni kujadili utekelezaji wa azimio la Umoja wa Mataifa la kusimamishwa kwa vita.

Mkutano huo pia utatoa rasmi amri ya wanajeshi 15,000 kuelekea kusini mwa Lebanon, kuchukua jukumu la eneo hilo kutoka kwa wapiganaji wa Hezbollah huku wakisubiri kikosi cha kimataifa kuwasili.

Duru ziliashiria kuwa mkutano huo, ambao pia utahudhuriwa na mawaziri wawili wa Hezbollah, huenda ukapendekeza kuwajumuisha wanamgambo wa Hezbollah katika jeshi la Lebanon.

Hezbollah wamegusia kuwa hawataweka kando silaha zao hadi pale wanajeshi wote wa Israel wataondoka kutoka ardhi ya Lebanon.

Mawaziri wa mambo ya kigeni kutoka Ufaransa, Uturuki, Malaysia na Pakistan pia wamewasili nchini Lebanon, kufanya majadiliano na waziri mkuu Fuad Sinora kuhusiana na kuwepo kwa jeshi hilo la kimataifa.

Wakati huo huo, meya wa mji wa Srifa nchini Lebanon amethibitisha kupatikana kwa maiti 32 kutoka katika mabaki ya jengo mmoja lililololipuliwa kwa mabomu.

Waookoaji walifanikiwa kuzitoa maiti hizo kutoka kwa vifusi vya jengo, lililipuliwa na Israél pale ilipodaiwa kuwa Hezbollah walitumia jengo hilo la ghorofa 15 kama kinga ya kufyatua makombora yao.

Na huko Jerusalem, naibu wa waziri mkuu Shimon Peres amesema seriali ya Israel haitasambaratika kufuatia shutma kuwa ilifeli katika harakati zake nchini Lebanon.

Peres alisema walifahamu vyema kuwa hawangeweza kuwaua wanamgambo wote wa Hezbolloh, lakini akasisitiza idadi ya waliofariki ni ufanisi mkubwa.

Waziri mkuu Ehud Olmert na maafisa wakuu wamekosolewa vikali baada ya vita hivyo vya mwezi mmoja nchini Lebanon.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW