Mpango wa kusitishwa mapigano Gaza unatarajiwa kuanza leo
23 Novemba 2023Hatua hiyo ni baada ya karibu wiki saba za vita.Hamas walisema mpango huo utaanza leo Alhamisi saa nne kamili asubuhi. Lakini Israel imesema mpango huo hautaanza hadi pengine kesho Ijumaa. Mshauri wa usalama wa taifa Tzachi Hanegbi amesema mawasiliano kuhusu kuwachiwa kwa mateka wao yanaendelea kupiga hatua.Wakizungumza mjini Tel Aviv jana usiku katika kikao cha pamoja cha waandishi habari Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, waziri Benny Gantz na Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant, wameapa kuwaleta nyumbani mateka wote na kuwaangamiza wanamgambo wa Hamas. Netanyahu amesema kuwa vita hivyo vitaendelea hadi watakapoyatimiza malengo yao. Chini ya mpango huo, mateka 100 wataachiwa kutoka Gaza kwa kubadilishana na wafungwa 300 wa Kipalestina wanaoshikiliwa nchini Israel. Aidha, malori yaliyobeba misaada ya dharura yataruhusiwa kuingia Ukanda wa Gaza ambako hakuna chakula, maji, umeme na dawa na vifaa vya matibabu.