Israel, Hamas wasaini mpango wa amani wa Gaza
9 Oktoba 2025
Rais wa Marekani Donald Trump amesema Israel na Hamas wametia saini awamu ya kwanza ya mpango wa amani ya Gaza. Kundi la Hamas linatarajiwa kuwaachilia huru mateka 'hivi karibuni' likisema mateka wa Israel walio hai watabadilishwa kwa karibu wafungwa 2,000 wa kipalestina. Israel nayo itawaondoa wanajeshi wake kwa njia iliyokubaliwa.
Msemaji wa serikali ya Israel ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba Israel inatarajia mateka wake wataanza kuachiwa Jumamosi. Msemaji huyo hakusema iwapo serikali inatarajia mateka wote 48 waliosalia, wanaoishi na waliokufa, wataachiliwa wote mara moja. Trump alisema Jumatano kwamba anaamini mateka wote walioshikiliwa huko Gaza, ikiwa ni pamoja na miili ya marehemu, "watarudi" Jumatatu.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu atakutana na baraza lake la mawaziri leo Alhamisi ili kuidhinisha mpango wa kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa huko Gaza, kwa mujibu wa vyanzo rasmi. "Kesho nitaitisha serikali ili kuidhinisha makubaliano hayo na kuwarudisha mateka wetu wapendwa nyumbani," Netanyahu alisema katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake Jumatano usiku.
Kundi la Hamas limesema katika taarifa yake kwamba "limefikia makubaliano ya kuvifikisha mwisho vita huko Gaza, kukomeshwa kwa uvamizi, kuingia kwa misaada ya kibinadamu na kubadilishana wafungwa".
Hama pia imemtaka Rais wa Marekani Donald Trump kuishinikiza Israel kutekeleza kikamilifu makubaliano hayo na "kutoiruhusu kukwepa au kuahirisha kutekeleza yale ambayo yamekubaliwa."
Mazungumzo yanaendelea Sharm el Sheikh nchini Misri
Tangazo la Trump linakuja wakati viongozi wa Hamas na Israel wakiendelea na mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja nchini Misri kuhusu pendekezo la amani lenye vipengele 20 lililozinduliwa na Trump kumaliza vita vilivyodumu kwa miaka miwili.
Trump alisema katika tangazo hilo, "Hii ina maana kwamba mateka wote wataachiliwa hivi karibuni, na Israeli itaondoa wanajeshi wao kwa mstari uliokubaliwa kama hatua ya kwanza kuelekea amani yenye nguvu, ya kudumu na ya milele,"
Hamas kwa sasa inaaminika kuwa inawashikilia mateka 48 wa Israel iliowachukua wakati wa mashambulizi ya kigaidi ya Oktoba 7. Chini ya nusu ya mateka hao wanafikiriwa kuwa hai.
"Kwa msaada wa Mungu, tutawaleta wote nyumbani," Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema baada ya tangazo la Trump, akimaanisha mateka wa Israel.
Tangazo hilo pia linaweza kumaanisha ahueni kwa Wapalestina baada ya zaidi ya miaka miwili ya vita huko Gaza.
Hamas ilimtaka Trump na nchi wapatanishi kuhakikisha kuwa Israel inatekeleza upande wake wa makubaliano hayo. Marekani, Ujerumani na nchi nyingine kadhaa zinaichukulia Hamas kama kundi la kigaidi.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amezungumza na Rais wa Marekani Donald Trump, na wote wawili wamepongezana kwa "mafanikio ya kihistoria" ya kutia saini makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza ambayo yanajumuisha kuachiliwa huru kwa mateka wote. Ofisi ya Netanyahu imesema leo Alhamisi katika taarifa kwamba viongozi hao wawili walikubaliana kuendelea na ushirikiano wao wa karibu, na Netanyahu amemualika Trump kuhutubia Knesset.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameyakaribisha makubaliano ya Israel na Hamas yaliyotangazwa na Rais Trump kuhusu awamu ya kwanza ya mpango wake wa amani wa Gaza, akitoa wito kwa pande zote "kutii kikamilifu" masharti yake. Guterres amezihimiza pande zote mbili ziyaheshimu makubaliano yaliyoafikiwa.