1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Guterres aonya oparesheni kubwa ya kijeshi ya Israel, Gaza

Hawa Bihoga
26 Februari 2024

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametahadharisha kuwa operesheni kubwa ya kijeshi ya Israel katika mji wa Rafah, kusini mwa Gaza itaathiri zaidi shughuli za kupeleka misaada katika ukanda wa Gaza.

Baraza la Haki za Binadamu, UN | Katibu Mkuu Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: Gian Ehrenzeller/KEYSTONE/picture alliance

 Guterres pia amelalamikia jinsi Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilivyoshindwa kushughulikia vita vya Israel katika ukanda wa Gaza. Guterres amesema huenda kushindwa huko kukadhoofisha vibaya mamlaka ya chombo hicho. 

Akizungumza mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Katibu Mkuu Guterres amesema mji wa Rafah, ambako zaidi ya Wapalestina milioni 1.4 wamejihifadhi katika mahema, ndiyo ulikuwa kitovu cha operesheni za kiutu katika eneo hilo la Wapalestina.

Guterres amesema mashambulizi kamili dhidi ya mji huo siyo tu yatakuwa ya kuogofya kwa raia zaidi ya milioni moja wa Kipalestina wanaojihifadhi mjini humo, lakini pia yataathiri programu za misaada za umoja huo.

Matamshi yake yamekuja baada ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kusisitiza jana Jumapili kwamba nchi yake ilikuwa imedhamiria kufanya uvamizi wa ardhini Rafah, katika jaribio lake la kuliangamiza kabisaa kundi la Hamas, ambalo shambulizi lake la Oktoba 7 lilisababisha vita hivyo.

Soma pia:Watu 71 wauawa katika mashambulizi kusini, katikati mwa Gaza

Alisema kwamba mara tu baada ya kutokea kwa uvamizi huo, ushindi utapatikana ndani ya wiki chache tu, na kwamba uwezekano wa makubaliano ya kusitisha vita yanayojadiliwa mjini Doha, utachelewesha tu operesheni hiyo.

"Tukianza operesheni ya Rafah, awamu ngumu ya mapigano itakamilika baada ya wiki kadhaa, sio miezi, wiki kadhaa tu kukamilika." alisema Netanyahu

Aliongeza kuwa vikosi vya Israel vimeangamiza bataliani 18 kati ya 24 za Hamas. Na nne kati yake ziko Rafah.

"Hatuwezi kuacha ngome ya mwisho ya Hamas bila kuishughulikia. Ni wazi kwamba tunapaswa kufanya hivyo." Alisema

"Lakini elewa pia kwamba nimeliomba jeshi liwasilishe kwangu mipango ya uhamisho wa raia wa Palestina Gaza, na ngome za Hamas zilizosalia." Alimaliza katika sehemu ya hotoba yake kwa umma

Mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel yaigharimu Gaza

Vita hivyo ambavyo vimekuwa vikirindima kwa zaidi ya miezi minne vilizuka baada ya shambulio la Hamas la Oktoba 7, ambalo lilisababisha vifo vya takriban watu 1,160 nchini Israel, wengi wao wakiwa ni raia kwa mujibu wa maelezo ya serikali ya Israel.

Wakaazi wa Ukanda wa Gaza wakisafisha baada ya mashambulizi ya vikosi vya IsraelPicha: MOHAMMED ABED/AFP/Getty Images

Wapiganaji wa Hamas pia waliwachukua mateka Waisrael na wageni wapatao 250, na 130 kati yao wanaendelea kushikiliwa Gaza, wakiwemo 31 wanaodhaniwa kuuawa, kulingana na Israel.

Mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel yamesababisha vifo vya takriban watu 29,692, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, kulingana na ripoti ya hivi karibuni iliyotolewa Jumapili na wizara ya afya huko Gaza inayoendeshwa na Hamas.

Soma pia:Mzozo wa kifedha wa UNRWA kusababisha ukosefu zaidi wa utulivu?

Guterres amesisitiza Jumatatu kwamba "hakuna chochote kinachoweza kuhalalisha mauaji ya makusudi ya Hamas, kuwajeruhi, kuwatesa na kuwateka raia, matumizi ya unyanyasaji wa kingono, au kurusha roketi kiholela kuelekea Israel. Lakini ameongeza pia kwamba hakuna kinachohalalisha adhabu ya pamoja ya watu wa Palestina.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Mamlaka ya Wapalestina Mohammad Shtayyeh amejiuzulu wadhifa wake leo, akisema matukio ya hivi karibuni katika kanda, ikiwemo vita vya Gaza, vilikuwa sababu ya kujiuzulu kwake.

Hatua hiyo ambayo inaripotiwa kushinikiwa na Rais Mahmoud Abbas, inatajwa kuwa inalenga kutimiza lengo la mageuzi ya Mamlaka ya Wapalestina ili kuiwezesha kuitawala Gaza baada ya Vita.

Msafara mwingine wa malori ya misaada waingia Gaza

01:57

This browser does not support the video element.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW