1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel, Hamas zapinga waranti wa kukamatwa viongozi wao

21 Mei 2024

Israel na Hamas, zimepambana vikali kwenye eneo la Ukanda wa Gaza, huku pande zote mbili zikipinga kwa hasira hatua ya kutaka kukamatwa kwa viongozi wao iliyotangazwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa kivita, ICC.

Picha iliyounganishwa ya Benjamin Netanjahu na Yahya Sinwar
Benjamini Netanyahu (kushoto) na kiongozi wa Hamas, Yahya Sinwar.Picha: DEBBIE HILL/Pool via REUTERS/MAHMUD HAMS/AFP via Getty Images

Israel imeshutumu na kuitaja kama fedheha ya kihistoria, ombi linalomlenga waziri mkuu Benjamin Netanyahu na waziri wake wa ulinzi Yoav Gallant, huku kundi la Hamas likisema linalaani vikali hatua hiyo.

Netanyahu amesema anapinga na kuchukizwa na hatua ya mwendesha mashtaka  wa ICC kulinganisha kile alichokiita "Israel ya kidemokrasia na wauaji wa kundi la Hamas."

Khan alisema katika taarifa kwamba anatafuta waranti dhidi ya viongozi wa Israel kuhusiana na uhalifu ukiwemo mauaji ya kukusudia, maangamizi, mauaji na njaa.

Alisema Israel ilikuwa imetenda uhalifu dhidi ya ubinadamu wakati wa vita vilivyoanzisha na shambulizi la Hamas la Oktoba 7, kama sehemu ya mashambulizi mapana ya kimfumo dhidi ya raia wa Kipalestina.

Soma pia:Mwendesha mashtaka Mkuu wa Mahakama ya ICC anatafuta waranti wa kukamatwa viongozi wa Israel na Hamas 

Khan pia alisema viongozi wa Hamas, akiwemo Ismail Haniyeh mwenye makao yake nchini Qatar na kiongozi wa kundi hilo katika Ukanda wa Gaza Yahya Sinwar, wanabeba jukumu la uhalifu kwa matendo yaliofanya wakati wa shambulio la Oktoba 7.

Haya yanahusisha kuchukuwa watu mateka, ubakaji na vitendo vingine vya vurugu za kingono au mateso.

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC Karim KhanPicha: Peter Dejong/AP/picture alliance

Marekani, mshirika mkuu wa Israel, pia imelipinga ombi la ICC, huku Rais wa Marekani Joe Biden akilikosoa na kusema hakuna usawa kati ya Israel na Hamas.

Biden pia alikanusha shutuma katika Mahakama ya Umoja wa Mataifa, ICJ, ambapo Afrika Kusini imedai kuwa vita vya Israel Gaza ni vya mauaji ya kimbari.

"Kinachotokea sio mauaji ya halaiki," Biden aliiambia hafla ya Mwezi wa Urithi wa Kiyahudi wa Marekani katika Ikulu ya White House Jumatatu.

Afrika Kusini iliikaribisha hatua hiyo katika ICC, huku Ufaransa ikisema inaunga mkono uhuru wa mahakama hiyo "na mapambano dhidi ya kutowajibishwa katika hali zote".

Uingereza na Australia zimesema ombi hilo la Mwendesha mashtaka wa ICC halisaidii chochote, huku Ujerumani ikikubaliana na msemaji wa wizara yake ya mambo ya nje aliyesema kwamba waranti huo unatoa hisia ya uongo kuhusu usawa.

"Tutaenda wapi?! Wahoji raia waliokata tamaa

Mapigano yanaendelea bila kukoma, huku wanajeshi wa Israel wakipambana na Hamas katika mji wa kusini mwa Gaza wa Rafah, na vile vile katika maeneo mengine ya katikati na kaskazini.

ICC yaitunishia kifua Marekani

01:10

This browser does not support the video element.

Israel imepuuza upinzani wa kimataifa takriban wiki mbili zilizopita ilipotuma wanajeshi wake mjini Rafah, ambako raia waliokimbia mapigano kwingineko Gaza wamelundikana, na ambao jeshi la Israel limeutaja kama ngome ya mwisho ya Hamas.

Netanyahu ameapa kuendelea kupambana na Hamas hadi kulisambaratisha kundi kundi hilo na mateka wote waliosalia waachiliwe. Umoja wa Mataifa umesema zaidi ya Wapalestina 812,000 wamekimbia Rafah.

"Swali linalotusumbua ni: tutaenda wapi?" Alisema Sarhan Abu al-Saeed, 46, mkaazi wa Palestina aliyekata tamaa. "Kifo cha uhakika kinatukimbiza kutoka pande zote."

Mashahidi wameliambia shirika la habari la AFP kuwa vikosi vya jeshi la wanamaji la Israel pia viliishambulia Rafah, na madaktari waliripoti shambulio la anga kwenye jengo la makazi magharibi mwa mji huo.

Jeshi lilisema vikosi vya Israel "vinaendesha mashambulizi ya kulenga dhidi ya miundombinu ya kigaidi" mashariki mwa Rafah, ambapo vilipata "mashimo kadhaa" na "kuwaangamiza zaidi ya magaidi 130".

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW