1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel: Hatutaiacha Rafah ikiwa na miundombinu thabiti

Hawa Bihoga
3 Julai 2024

Vikosi vya Israel vimeshambulia kwa mabomu na kuendeleza mapigano na wanamgambo wa Hamas leo, huku maelfu ya Wapalestina wakitafuta eneo salama baada ya jeshi kutoa amri ya kuondoka eneo la kusini mwa Gaza.

Ukanda wa Gaza, Khan Yunis | Mji ulioharibiwa na vita
Mji wa Khan Yunis Ukanda wa Gaza ulioharibiwa vibaya na mashambulizi ya Israel.Picha: Ali Jadallah/Anadolu/picture alliance

Helikopta na droni zimeshuhudiwa katika anga la wilaya Shujaiya huko Gaza huku milio ya risasi ikisikika katika mitaa, siku kumi baada ya Waziri Mkuu wa Israel Benyamin Netanyahu kusema "awamu kali" ya vita ilikuwa imefika ukingoni.

Mapema leo jeshi la Israeli lilifanya tena mashambulizi ya anga na ardhini dhidi ya wanamgambo wa Hamas katika wilaya hiyo ya Shujaiya.

Soma pia:Israel yaendeleza mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza

Mkuu wa jeshi amekiri kuwa jeshi la Israel lina safari ndefu ya kulisambaratisha kabisa kundi la Hamas kufuatia shambulio lake la Oktoba 07, na kuwarejesha nyumbani mateka wanaoshikiliwa na wanamgambo hao wa Kipalestina.

"Juhudi zetu za sasa, na sababu ya sisi kuwa hapa kufanyakazi wiki hadi wiki, zinaelekezwa katika kusambaratisha miundombinu ya kigaidi." Halevi aliwaambia wanajeshi alipowatembelea katika kufanya ukaguzi katika baadhi ya kambi za jeshi.

Aliongeza kwamba "kampeni hii ni ya muda mrefu kwa sababu hatupaswi kuiacha Rafah ikiwa na miundombinu thabiti."

Jeshi la Israel limesema kikosi chake cha anga kimeshambulia zaidi ya maeneo 50 iliyoyataja kuwa ni ya "kigaidi" ndani ya saa 24 huku kikosi cha ardhini kikiendeleza mashambulizi kwenye mahandaki na kukamata silaha kadhaa zinazodaiwa ni za wanamgambo ikiwemo bunduki.

Amri ya raia kuondoka eneo la kusini

Jeshi hilo la Israel ambalo lilitoa amri ya raia kuondoka katika eneo la Shujaiya wiki moja iliopita, limetoa pia amri kama hiyo katika maeneo yenye idadi kubwa ya watu karibu na mji wa Khan Yunis na kusini mwa Rafah, hatua ambayo imezusha wasiwasi wa kuzuka kwa mapigano makali zaidi katika eneo hilo.

Maelfu ya Wapalestika kwa mara nyingine tena wameingia barabarani kusaka pahala salama kwa ajili ya kujihifadhi na familia zao kwenye Ukanda huo ambao umeharibiwa vibaya kwa mashambulizi ya kisasi ya Israel.

Soma pia:Raia wa Gaza watafuta makao baada ya amri ya kuondoka kusini mwa Gaza kutolewa

Umoja wa Mataifa Umeonya kwamba vita hivyo vilivyodumu kwa takriban miezi tisa sasa vimesababisha "maafa makubwa ya kibinaadamu" na kwamba amri ya hivi karibuni ya kuwahamisha raia imewatumbukiza zaidi Wapalestisna "katika dimbwi la mateso."

Idadi ya vifo na majeruhi yaongezeka Ukanda wa Gaza

02:51

This browser does not support the video element.

Wizara ya afya Gaza inayoongozwa na Hamas imesema katika taarifa yake kwamba zaidi ya watu 37,953 wameuwawa na wengine 87,266 wamejeruhiwa katika mashambuzlizi ya Israel tangu kuzuka kwa vita hivyo mnamo oktoba 07.

Katika hatua nyingine Kamanda Mkuu wa kundi la Hezbollah ambae alikuwa anahusika na oparesheni za mpakani kunakoshuhudiwa makabiliano makali baina ya Lebanon na Israel yakienda sambamba na vita vya Gaza, ameuwawa katika shambulio la vikosi vya Israel.

Hezbollah haijazungumzia chochote kuhusu kifo cha kamanda wake, lakini kumeripotiwa mashambulizi makubwa ya anga yakitajwa ni yakulipiza kisasi kufuatia kifo cha kamanda wake huyo mwenye cheo cha juu.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW