Israel, Hezbollah zashambuliana baada ya mazungumzo Marekani
15 Aprili 2026
Israel na Hezbollah zimekabiliana tena kwa risasi leo Jumatano. Shirika la habari la Lebanon, NNA, limeripoti vifo kufuatia mashambulizi ya anga ya Israeli usiku kucha na mapema Jumatano kusini mwa Lebenon.
Jeshi la Israeli halijatoa kauli yoyote kuhusu ripoti hiyo, lakini limesema ni operesheni za ardhini zilizolengwa pekee ambazo zilikuwa zikiendelea kusini mwa Lebanon, zikilenga kulinda idadi ya watu kaskazini mwa Israel.
Wanamgambo wa Hezbollah wanaoungwa mkono na Iran walidai kuhusika na mashambulizi kadhaa kaskazini mwa Israeli, ambapo ving'ora vya kutoa onyo vilisikika. Jeshi la Israel limesema limerekodi takriban makombora 30 kutoka Lebanon mapema Jumatano.
Jumanne jioni, balozi wa Lebanon nchini Marekani, Nada Hamadeh Moawad, na mwakilishi wa Israel huko Washington, Jechiel Leiter, walifanya mazungumzo.
Kwa mujibu wa vyanzo vya Marekani, mazungumzo ya moja kwa moja yanatarajiwa kuendelea na yanaweza kusababisha makubaliano ya amani kamili.