Israel yamuua kamanda wa Hezbollah mjini Beirut
7 Mei 2026
Maafisa wa Israel wamesema jeshi la anga la nchi hiyo limefanya shambulio katika kitongoji kimoja mjini Beirut huko Lebanon kwa mara ya kwanza tangu kusitishwa kwa mapigano wiki tatu zilizopita, likimlenga kamanda wa kikosi cha Radwan cha Hezbollah.
Katika taarifa ya pamoja, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na Waziri wa Ulinzi, Israel Katz wamesema operesheni hiyo ilikuwa na lengo la "kumwangamiza " kamanda huyo aliyefahamika kwa jina la Malek Balut.
Mapema vyombo vya habari vya Israel viliripoti kuuliwa kwa kamanda huyo, naibu wake na wapiganaji wengine kadhaa katika shambulio hilo. Baadaye vyanzo vya habari vya Hezbollah vimethibitisha pia kifo cha kamanda huyo kwa shirika la habari la dpa.
Kulingana na maafisa wa Israel, Marekani iliarifiwa kabla ya kufanyika shambulio hilo na kuidhinisha operesheni hiyo.