Israel inaendeleza mashambulizi yake katika ukanda wa Gaza
9 Novemba 2023Vyombo vya habari vimeripoti kuwa Israel imeendeleza mashambulizi yake makubwa katika Ukanda wa Gaza usiku wa kuamkia leo na kuwauwa mamia ya Wapalestina katika kambi ya wakimbizi ya Jabalia Kaskazini mwa Gaza na Sabra Magharibi mwa ukanda huo.
Mlipuko mkubwa pia uliripotiwa karibu na Hospitali ya al-Shifa katikati ya jiji la Gaza mapema leo.
Idadi ya vifo katika ukanda wa Gaza imeongezeka
Kulingana na takwimu mpya za wizara ya afya katika ukanda wa Gaza unaotawaliwa na Hamas, idadi ya vifo katika eneo hilo imeongezeka na kufikia zaidi ya watu 10,600, wakiwemo zaidi ya watoto 4,300, huku maelfu ya wengine hawajulikani walipo na wengine kudhaniwa kuwa wamekufa chini ya vifusi vya majengo yalioporomoka kutokana na mashambulizi ya Israel.
Hali katika hospital ya Ulaya huko Khan Yunis yatajwa kuwa janga
Tom Potokar daktari mkuu wa upasuaji kutoka shirika la kimataifa la msalaba mwekundu, ametaja hali katika hospitali ya Ulaya huko Khan Yunis Kusini mwa Gaza kuwa "janga". Potokar ameliambia shirika la habari la AFP kwamba katika muda wa masaa 24, ameshuhudia wagonjwa watatu wakiwa na funza katika vidonda vyao.
Umoja wa Mataifa na WHO zasema msaada uliopelekwa Gaza hautoshi
Umoja wa Mataifa na Shirika la Afya Duniani - WHO wamesema kuwa bidhaa za dharura za matibabu zilifikishwa katika hospitali kuu ya Gaza, Al-Shifa hapo jana Jumatano, ikiwa ni mara ya pili kupelekwa kwa msaada huo tangu kuanza kwa vita hivyo. Zimeonya kuwa msaada huo bado hautoshi kushughulikia mahitaji makubwa ya raia katika eneo hilo.
Mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel katika ukanda wa Gaza, yametokana na shambulizi la kushtukiza la kundi la wanamgambo wa Hamas la Oktoba 7 Kusini mwa Israel ambapo zaidi ya watu 1400 waliuawa na wengine zaidi ya 200 kuchukuliwa mateka.
Mazungumzo ya kusitisha vita yanaendelea
Mazungumzo yanaendelea ili kufikia makubaliano ya usitishaji wa vita kwa siku tatu kuwezesha kupelekwa kwa msaada wa kibinadamu katika ukanda wa Gaza ili kubadilishana na kuachiwa huru kwa mateka wa Israel wanaoshikiliwa na wanamgambo wa Hamas.
Soma pia:Israel yadai kuuzingira mji wa Gaza huku idadi ya vifo ikiongezeka
Hayo ni kwa mujibu wa maafisa wawili kutoka Misri, mmoja kutoka Umoja wa Mataifa na mwanadiplomasia wa Magharibi, waliozungumza kwa masharti ya kutotambulishwa kwasababu ya juhudi nyeti za kidiplomasia.
Soma pia:Kasi ya raia wa Palestina wanaotoroka eneo la mapigano kaskazini mwa Gaza imeongezeka
Mpangilio huo utawezesha kutolewa kwa misaada zaidi, ikijumuisha kiwango kidogo cha mafuta kuingia katika eneo lililozingirwa la ukanda wa Gaza ili kupunguza madhila ya Wapalestina milioni 2.3 waliokwama katika eneo hilo.
Kulingana na maafisa hao wawili, mazungumzo hayo yanasimamiwa na Qatar, Misri na Marekani.