1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Israel yaishambulia tena Hospitali ya Al-Shifa

18 Machi 2024

Vikosi vya jeshi la Israel, vimefanya mashambulizi mapya katika hospitali ya al Shifa iliyoko Gaza City ikidai kwamba wanamgambo wa Hamas wanaitumia hospitali hiyo kama ngome yake.

Mzozo wa Mashariki ya Kati | Hospitali ya Al-Shifa mjini Gaza
Wanajeshi wa Israel wakiwa wamesimama nje ya Hospitali ya Shifa katika Jiji la Gaza, Jumatano, Novemba 22, 2023.Picha: Victor R. Caivano/AP Photo/picture alliance

Kulingana na jeshi hilo la Israel, operesheni hiyo inafuatia taarifa za kiintelijensia zinazoonyesha maafisa waandamizi wa Hamas wanalitumia eneo hilo kuendesha shughuli zao. 

Msemaji mkuu wa jeshi la Israel Daniel Hagari amesema jeshi la nchi hiyo limeanzisha kile ilichoita operesheni ya kijeshi iliyoratibiwa kikamilifu katika baadhi ya maeneo ya jengo la hospitali hiyo. Amesema wanamgambo waandamizi wa Hamas wamejikusanya upya na wamekuwa wakifanya mashambulizi kutokea hapo. 

"Wanajeshi wetu wamepata mafunzo maalumu ya kuwaandaa kwa ajili ya mashambulizi kwenye mazingira tete wanayoweza kukutana nayo. Hivi ni vita dhidi ya Hamas na sio watu wa Gaza." Hata hivyo Hagari hakuthibitisha madai hayo.

Soma pia:Israel yaendesha operesheni ndani ya hospitali Gaza 

Amesema wagonjwa na watoa huduma wanaweza kubakia kwenye eneo hilo na kuliandaliwa njia salama kwa ajili ya raia kuondoka. Israel kwa mara ya kwanza iliishambulia hospitali hiyo kubwa kabisa kwenye Ukanda wa Gaza mwezi Novemba ikitoa madai kama haya ya kwamba Hamas inalitumia eneo hilo kupanga na kuagiza mashambulizi dhidi yake na kuwatumia watu waliojificha humo kama kama ngao ya vita.

Wizara ya Afya ya Gaza imesema jeshi limelishambulia jengo la upasuaji mapema leo Jumatatu, wakifyatua risasi kutokea lango kuu la kuingilia hospitalini hapo. Kulingana na wizara hiyo, karibu watu 30,000 waliokimbia makazi yao kutokana na vita wanajihifadhi kwenye hospitali hiyo na hivi sasa wana mashaka makubwa baada ya Israel kuanzisha mashambulizi hayo.

Wanajeshi wa Israel wakipiga doria karibu na kambi ya Hospitali ya Al Shifa katika Jiji la Gaza, huku kukiwa na operesheni ya ardhini inayoendelea ya jeshi hilo dhidi ya kundi la Hamas, Novemba 22, 2023.Picha: Ronen Zvulun/Reuters

Soma pia: Mamia ya wagonjwa waondoka hospitali ya Al-Shifa

Katika hatua nyingine, Israel imesema inajiandaa kupeleka ujumbe wake huko Qatar hii leo utakaoshioriki mazungumzo ya kusitisha mapigano, hii ikiwa ni kulingana na tovuti ya habari ya Ynet. Inaripotiwa kwamba Mkuu wa shirika la kijasusi la Israel, Mossad, David Barnea ni miongoni mwa wajumbe hao.

Shirika la Habari la AP limeripoti kwamba ujumbe huo uliruhusiwa kushiriki mazungumzo hayo baada ya mkutano wa Baraza la Usalama la Israel pamoja na lile la Vita jana Jumapili iliyotoa mamlaka kwa wajumbe hao.

Kwenye mazungumzo hayo ya mjini Doha, washiriki wa mazungumzo kutoka Qatar, Misri na Marekani watarajaribu kukubaliana kusogeza mbele usitishwaji wa muda wa mapigano pamoja na makubaliano ya kuwaachia huru mateka wa Israel wanaoshikiliwa huko Gaza pamoja na wafungwa wa Palestina wanaozuiwa Israel.

Huku hayo yakiendelea, shirika la kimataifa lisilo la kiserikali la kutoa msaada  Oxfam limeishutumu Israel kwa kuzuia kwa makusudi kuingizwa kwa misaada ya kiutu katika Ukanda wa Gaza. Kwenye ripoti iliyochapishwa hii leo, shirika hilo limesema kwamba sheria zisizo halali za ukaguzi za Israel zimekwamisha kwa takriban siku 20 malori yaliyobeba misaada.

Shirika hilo aidha limelaani mashambulizi dhidi ya wafanyakazi na vituo vinavyotumiwa kutoa misaada ya kiutu, pamoja na misafara inayopeleka misaada hiyo.

Soma pia: Biden asema usitishaji mapigano Gaza unakaribia

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW