ISRAEL ISIHATARISHE MAZUNGUMZO:
19 Desemba 2003Matangazo
WASHINGTON: Marekani imeionya Israel kutochukua hatua za upande mmoja zitakazozuia majadiliano yanayoungwa mkono na Washington kutafuta amani ya kudumu katika Mashariki ya Kati.Marekani imetoa muito kwa mawaziri wakuu wa Israel na Wapalestina kukutana upesi,bila ya kuweka masharti.Hatua hiyo imechukuliwa baada ya waziri mkuu wa Israel Ariel Sharon siku ya Alkhamis kutamka kuwa Israel katika kipindi cha miezi kadhaa,itachukua hatua za kujitenga kutoka maeneo ya Wapalestina,ikiwa majadiliano ya maana hayatoanzishwa.Waziri mkuu wa Wapalestina Ahmed Qurie amejibu kwa kusema kuwa amevunjika moyo kwa kile alichokiita "kitisho" cha Sharon.Akisema yupo tayari kuwa na mapatano ya kudumu na kuumaliza mzozo,Qurie alisisititza kuwa majadiliano yanaweza kuanza moja kwa moja.
