1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel yathibitisha kifo cha kamanda wa ngazi ya juu Hamas

Hawa Bihoga
15 Julai 2024

Jeshi la Israel limesema Kamanda wa ngazi za juu wa Hamas Rafa Salama amethibitishwa kuuwawa katika shambulio la anga, ambapo lililenga kambi ya wakimbizi na kusababisha vifo vya watu takriban 90.

Gaza | Nuseirat | Jengo la shule ya UNRWA
Sehemu ya jengo la UNRWA likiwa limeharibiwa vibaya baada ya shambulio la Israel.Picha: Omar Ashtawy/APA/ZUMA/picture alliance

Katika shambulio hilo la mwishoni mwa juma lililopita, Salama pamoja na Kiongozi wa tawi la kijeshi la Hamas Gaza Mohammed Deif, wawili hao wanatajwa kuwa wapangaji wakuu wa shambulio la Oktoba 7 ndani ya ardhi ya Israel na ambalo lilisababisha mashambulizi ya kulipiza kisasa ya Israel na kupelekea hasara kubwa ikiwemo vifo vya raia.

Mbali ya taarifa ya jeshi la Israel kuthibitisha kuwawa kwa Salama lakini haikutoa taarifa za kina kuhusu Mohammed Deif.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu hapo awali alisema kuwa hakuna taarifa kamili juu ya Deif, wakati Afisa wa Hamas katika mji mkuu wa Lebanon Beirut alisema kwamba yupo imara licha ya shambulio la bomu la Israel ambalo lililenga kumuua.

Israel imemtaja Salama kama mshirika wa karibu na Deif na kwamba kifo chake kitaathiri vibaya uwezo wa kijeshi wa Hamas.

Aidha jeshi la Israel limeongeza kuwa Salama aliongoza kikosi cha Khan Younis kusini mwa Gaza na alihusika na mashambulizi mengi ya roketi yaliyofanywa dhidi ya Israeli katika miaka ya hivi karibuni.

Bado Israel inaendeleza mashambulizi yake katika kambi kadhaa za wakimbizi wa Kipalestina ambao wamekimbia mapigano katika maeneo mengine.

Kundi la Hamas limesema kwamba  katika shambulio la jana Jumapili kwenye shule ya Nuseirat ambayo inatumika kama kambi ya wakimbizi kwa sasa limeuwa takriban watu 15.

Soma pia:Miili 60 yafukuliwa Gaza baada ya shambulizi la Israel

Jeshi la Israel hapo awali lilisema linalenga wapiganaji kadhaa wa kundi la itikadi kali la Palestina katika eneo la shule ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi wa Palestina (UNRWA), ambalo wanasema lilikuwa linatumiwa na Hamas kama maficho na kambi ya operesheni.

Baadhi ya Wapalestina wamelitaja kuwa shambulio hilo lilikuwa baya zaidi na kama la kushtukiza Yamen Abu Suleiman, alisema kulikuwa na majeraha makubwa kwa waokoaji wa shirika la Walinzi wa kiraia.

"Baadhi yao wapo mahututi na wengine kwa bahati mbaya walikatwa viungo vyao, ni jambo baya na lisiloelezeka. Raia pia walijeruhiwa, baadhi yao waliungua na moto na wengine walikatwa viungo kama miguu na mikono, kwa kifupi ni uhalifu."

Hamas kujiondoa kwenye mazungumzo?

Katika hatua ya kutafuta suluhu ya kusitisha mapigano katika eneo la Ukanda wa Gaza afisa mmoja wa Hamas amaesema kundi hilo la wapiganaji wa Kipalestina linajiondoa katika  mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza katika wakati ambapo Israel imeendeleza mashambulizi.

Kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh na kiongozi wa kundi la Islamic Jihad Ziyad Al Nakhalaj wakijadili mapendekezo ya kusitisha mapigano GazaPicha: HAMAS MEDIA OFFICE/REUTERS

Afisa huyo akimnukuu Kiongozi Mkuu wa Hamas mwenye makao yake nchini Qatar Ismail Haniyeh alisema msingi wa kufikia uamuzi huo ni pamoja na ukosefu wa umakini wa Israel, kuhairisha na kuzuiwa kwa mambo ya msingi pamoja na mauaji yanayoendelea dhidi ya raia.

Soma pia:Hamas yakanusha kujiondoa kwenye mchakato wa mazungumzo

Hata hivyo, kulingana na afisa huyo, Haniyeh aliwaambia wapatanishi wa kimataifa Hamas iko tayari kuanza tena mazungumzo wakati serikali ya Israel itakapoonesha umakini katika kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na makubaliano ya kubadilishana wafungwa.

Mazungumzo hayo yaliyosimamiwa na Qatar na Misri, kwa msaada wa Marekani, kwa miezi kadhaa yalijaribu kufikia lengo la kusimamisha mapigano yanayoendelea, lakini lengo hilo halikufua dafu.